Na Mwandishi Maalum, Dar es Salaam
Tanzania imesisitiza kuendeleza jitihada za upatikanaji wa haki na fursa sawa kijinsia ikiwa ni pamoja na haki za makundi maalum ya jamii.
Hayo yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam katika kikao kilichowakutanisha Waasisi wa Umoja wa Jumuiya za Wanawake katika Nchi Huru za Afrika (PAWO) na Wizara ya Afya, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii.
Akifungua kikao hicho kwa niaba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dk. John Jingu amesema Serikali imeendelea kuratibu juhudi za wadau kuhakikisha usawa wa jinsia unafikiwa katika nyanja zote hapa nchini.
Amesema Tanzania ni miongoni mwa Mataifa yaliyo mstari wa mbele katika kuchochea misingi ya usawa wa kijinsia na itaendelea kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha haki za binadamu zinazingatiwa katika nyanja zote.
Ameongeza kuwa kuna hatua za makusudi za kuwajengea uwezo Wanawake ili wanufaike na fursa za kiuchumi ili kufikia Usawa wa Kijinsia kupitia Mikakati na Sera zinazosisitiza uwezeshaji wanawake kiuchumi.
“Suala la usawa wa kijinsia ni miongoni mwa ajenda muhimu za maendeleo kitaifa na kimataifa utekelezaji wake unagusa nyanja mbalimbali zikiwemo Mikataba ya kikanda na kimataifa,”alisema Dk. Jingu.
Dk. John Jingu amesisitiza kuwa Msukumo mkubwa unawakwa katika suala la uingizaji wa masuala ya kijinsia katika Sera, na Programu za kisekta, uwezeshaji wanawake, kuzuia ukatili wa kijinsia ikiwa msingi wa usawa wa kijinsia nchini.
Aidha, Dk. Jingu amefafanua kuwa Serikali imezingatia umuhimu wanawake kupata fursa ya kushiriki katika ngazi mbalimbali za maamuzi na uongozi katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Waasisi wa Umoja wa Jumuiya za Wanawake katika Nchi Huru za Afrika (PAWO) Bibi Leah Lupembe ameishukuru Serikali ya Awamu ya sita kwa kuendelea kuwatumia waasisi wa Uhuru wa Tanganyika (Tanzania Bara) kutoa ushauri wa masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya wanawake na usawa wa kijinsia.
Wakizungumza kwa wakati tofauti katika kikao hicho baadhi ya Waasisi na watendaji PAWO wamesema kuwa wametumikia Taifa katika sekta mbalimbali na kutoa mchango mkubwa katika sekta hizo hivyo, wataendelea kushirikana na Serikali kwa maoni ya kuboresha mipango ya Maendeleo.