Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Hadija Kanyama na Rajan Ally wameibuka washindi katika mashindano ya kumtafuta mrembo wa Tanzania kwa watu wenye uziwi hivyo wataiwakilisha nchi katika mashindano ya kimataifa yanayotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Mashindano hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini yameandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA).
Akizungumza wakati wa mashindano hayo Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa Dk. Emmanuel Ishengoma ambaye alimwakilisha Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, amesema ni fursa nzuri kwa watu wenye uziwi kuonyesha vipaji vyao.
“Kila mmoja ana kipawa cha ziada, mtu anaweza kuwa na ulemavu wa macho au kushindwa kusikia lakini akawa na kipaji. Washiriki wote ni wazuri na Tanzania inaweza kutoa mshindi wa Afrika,” amesema Dk. Ishengoma.
Naye Mkurugenzi wa KISUVITA, Habibu Mrope, amesema wamekuwa wakikaribishwa katika mataifa mbalimbali kushiriki mashindano kama hayo lakini walikuwa wakishindwa kutokana na changamoto mbalimbali.
“Tuliangalia namna ya kusukuma jambo hili lisiendelee kulala ndiyo maana tukawa na mashindano haya. Wapo viziwi warembo na wanafanya vizuri kwahiyo tunaamini hata katika mashindaano ya kimataifa Tanzania tutafanya vizuri,” amesema Mrope.
Aidha amesema washindi watakabidhiwa zawadi zao mwezi ujao ambapo mshindi wa kwanza atakabidhiwa samani na fedha taslimu Sh milioni moja wakati mshindi wa pili atakabidhiwa Sh milioni moja.
Kwa upande wao Hadija na Rajan wameahidi kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
“Sitabweteka na taji la Miss Tanzania bali nimejiwekea misingi ya kuja kufanya vizuri zaidi kwenye mashindano ya Afrika,” amesema Hadija.
Mshiriki mwingine Caroline Mwakasaka aliyeibuka mwanamitindo bora amesema malengo yake ni kuwa mwanamitindo wa kimataifa.
“Niliwahi kushiriki mashindano miaka ya nyuma lakini sikukata tamaa ndiyo maana nikaendelea kushiriki ili kuuhakikishia umma kwamba ulemavu si kikwazo cha kushiriki kwenye urembo na sanaa,” amesema Caroline.
Katika mashindano hayo kituo hicho pia kilitoa tuzo kwa watu mbalimbali kwa kutambua mchango wao katika kuunga mkono juhudi zinazofanywa na viziwi katika shughuli zao za kila siku.