28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Makala|PROF. NDOMBA APANIA DIT KUWA KITOVU CHA MAFUNZO KWA VITENDO

Na Regina Kumba, DIT

”Tuna mpango wa kuanza kutoa Shahada ya Uzamivu katika Teknolojia yaani PhD in Technology na lengo letu ni kutayarisha wataalamu wa Kitanzania waliobobea katika teknolojia. Tutaanza kufundisha wanafunzi wa Phd hivi karibuni”, anasema Mkuu wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), Profesa Preksedis Ndomba.

Anasema hayo wakati wa hafla ya kutangaza kampuni nne za wanafunzi wa Taasisi hiyo zilizoshinda katika tenda ya kuandika maandiko ya miradi inayotekelezwa katika programu maalumu iitwayo Mafunzo kwa Vitendo (Teaching Factory).

Prof. Ndomba akiwa katika picha ya pamoja na wanafunzi walioshiriki kuandika andiko la miradi mwaka huu.

Kampuni hizo ni Clem Construction Company Limted inayohusika na masuala ya ujenzi, Meyu Electrical Company Limited and Silver Light ya masuala ya umeme, DarTech Solutions Limited inayoshughulikia masuala ya kielektroniki na mawasiliano ya simu na Techlads inayohusika na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Profesa Ndomba anawapongeza wanafunzi ambao kampuni zao zimeshinda katika kuandaa maandiko kwa ajili ya Teaching Factory kwa mwaka 2020/2021. Anasema kulikuwa na washiriki zaidi ya 80 kwa mwaka huu na washiriki wamekuwa wakiongezeka kila mwaka.

”Tuongeze bidii katika kushiriki katika programu hii. Vigezo vya tenda vilivyowekwa ni vya kiushindani, ni vya kushindana huko mtaani, siyo kushindana tu kitaaluma. Vigezo hivi vinataka mwanafunzi kuzingatia mambo mengi yaliyopo katika tenda kama zile za kawaida mfano kuipia kodi na tozo mbalimbali kama BRELA, NEMC na halmashauri,” anasema.

Profesa Ndomba anasema kuwa DIT imepanga kuwa Tasisi inayotoa viwango vya juu vya elimu ya ufundi iliyojikita katika kutatua matatizo ya jamii, ikiwemo kuanzisha mafunzo hayo ya digrii ya juu kabisa ya masuala ya teknolojia.

Akifafanua kuhusu dhana ya programu hiyo ya Mafunzo kwa Vitendo (Teaching Factory), Profesa Ndomba anasema Teaching Factory ilianzishwa mwaka 2016 lakini utekelezaji wake ulianza rasmi mwaka 2019 na programu hiyo imeleta mageuzi makubwa kwa wahadhiri na wanafunzi katika kuendeleza ujuzi na maarifa  ya teknolojia, ubunifu, ujenzi, usindikaji na ufungaji wa umeme na utengenezaji wa mitambo.

Prof. Ndomba akitunuku cheti cha ushindi wa mradi kwa mmoja wa wanafunzi walioshinda.

Profesa Ndomba anasema chini ya programu hiyo, wahitimu wa DIT wanapewa ujuzi na maarifa ambayo ni rahisi kutumika katika soko. Anasema programu hiyo inatekelezwa kulingana na Dira ya DIT ya kuwa kitovu cha kutoa elimu ya ufundi nchini katika kutatua matatizo ya jamii. Pia programu hiyo inaenda sambamba na Mwelekeo wa DIT wa kutoa elimu bora ya ufundi kupitia mafunzo, utafiti na maendeleo ya teknoloja yanayotakiwa.

”Kupitia Teaching Factory Tasisi yetu imeweza kutoa wahitimu walioiva walioajiriwa katika kampuni na viwanda mbalimbali na wanatoa mchango mkubwa katika kutekeleza ajenda ya Serikali ya kuwa nchi ya viwanda. Katika kutekeleza programu hii Tasisi imeongeza bajeti kwa ajili ya vifaa vya kufundishia kutoka Shilingi milioni 150 hadi Shilingi milioni 500,” anasema Profesa Ndomba.

Miaka ya nyuma vifaa vya kufundishia vilivyotumiwa na wanafunzi katika kutayarisha, kutengeneza, kujenga majengo au kubuni miradi, baadaye vilibomolewa, kuharibiwa au kuteketezwa. 

Ni wazi katika utaratibu huo kulikuwa na matumizi yasiyo mazuri ya fedha za umma, kwani miradi hiyo ya ubunifu haikutumika kwa matumizi halisi ya jamii. Lakini, baadaye DIT iliamua kutumia vizuri na kwa uangalifu vifaa vya kufundishia ili kutatua matatizo halisi ya chuo na jamii kwa ujumla. 

Aidha, Profesa Ndomba anasema kwa miaka mingi miradi ya Teaching Factory ilikuwa inabuniwa na menejimenti na kutekelezwa na wahadhiri na wanafunzi na baadhi ya miradi hiyo ni ukarabati wa barabara za Taasisi, ujenzi wa maaabara katika Idara Uhandisi, ujenzi, upanuzi wa maktaba, uzalishaji wa sabuni, utengenezaji wa vipukusi (kwa idhini ya TMDA), utengenezaji wa mashine za kunawia mikono na utengenezaji wa mashine mbalimbali.

”Lakini tangu mwaka wa masomo wa 2019/2020 menejimenti iliamua miradi ya Teaching Factory iwe inabuniwa na wanafunzi na lengo ni kuwawezesha kupata ujuzi na maarifa ya kukabiliana na  mazingira halisi ya kazi baada ya kuhitimu masomo,” anasema Profesa Ndomba.

Prof. Ndomba (wa pili kulia) akiwa na wanafunzi pamoja na wafanyakazi w DIT katika moja ya mashine iliyobuniwa na kutengengenezwa DIT.

Anasema kuna mambo kadhaa yaliyonyanyua na kuboresha utekelezaji ya Teaching Factory na mojawapo ni ongezeko la ziara za viwandani. Hivi sasa ziara viwandani zinafanywa kila wiki na jambo hilo limewezekana baada ya chuo hicho kununua basi kubwa. 

Mpaka sasa DIT ina mabasi mawili ambayo yanafanya safari za mara kwa mara viwandani kupeleka wanafunzi hivyo kufanya ziara za viwandani kuwa sehemu ya utamaduni wa wanafunzi wa DIT. 

DIT pia imeanzisha Kamati ya Kusimamia Teaching Factory yenye wajumbe sita wakiongozwa na Dk Sosthenes Karugaba.

Ndomba anatoa shukrani kwa Serikali kwa kuwezesha taasisi hiyo kutekeleza mipango na miradi yake mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa dhana hiyo ya Teaching Factory. 

MWANDISHI WA MAKALA HAYA NI AFISA UHUSIANO WA TAASISI YA TEKNOLIJIA DAR ES SALAAM (DIT)

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles