Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Tanzania imekuwa nchi ya kwanza miongoni mwa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kusaini mkataba wa kuanzishwa kituo cha huduma za kibinadamu na oparesheni za dharura za kanda.
Akizungumza mapema hii leo Februari 23, 2023 wakati wa hafla ya utiaji saini iliyofanyika jijini Dodoma Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, George Simbachawene amesema, Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) zimeendelea kushirikiana, katika masuala ya usimamizi wa maafa kupitia Kamati ya Mawaziri wenye dhamana ya Usimamizi wa Maafa.
Amesema miongoni mwa hatua zilizochukuliwa katika kuendeleza ushirikiano ni kuanzisha Kituo cha Huduma za Kibinadamu na Operesheni za Dharura cha Kikanda ambacho kipo Nacala, Jimbo la Nampula nchini Msumbiji. Kituo kilichozinduliwa na Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mheshimiwa Filipe Nyusi Juni 21, 2021.
“Lengo la kuanzisha Kituo hicho ni kusimamia masuala ya huduma za misaada ya kibinadamu kwa Nchi Wanachama zitakazokumbwa na maafa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusimamia na kuratibu utekelezaji wa shughuli za usimamizi wa maafa,” amesema.
Aliendelea kusema kuwa, mkataba huo umepitishwa na kamati zote zinazohusika ikiwemo Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa maafa Aprili, 2022 Lilongwe, Malawi; Kamati ya Mawaziri wanaohusika na usimamizi wa sheria na Wanasheria Wakuu Julai, 2022 Lilongwe Malawi; na Baraza la Mawaziri katika mkutano wa kawaida uliofanyika Agosti, 2022 Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali uliofanyika Agosti 17 na 18, mwaka jana Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo uliidhinisha Mkataba huu na kuelekeza kuwa usainiwe na Mawaziri wanaohusika katika usimamizi wa maafa.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu, Dk. John Jingu alisema jitihada hizi zilianzishwa kwa sababu, masuala ya majanga hayana mipaka na yanahitaji jitihada za pamoja na kushugulika kwa pamoja katika usimamizi.
Awali, mwakilishi kutoka sekretariati ya nchi hizo Mwanasheria Dk. Phiness Matto, alisema, Mkataba huu umekuja katika wakati muhimu ambapo kituo hiki kitakuwa na jukumu kubwa la kufanya uratibu, kutambua na kushughulikia athari zote kadiri itavyowezekana.
“Natoa Pongezi kwa Tanzania kuwa nchi ya kwanza ku sign mkataba huu na tunategemea nchi 11 kusaini mkataba huu,” amefafanua Dk. Matto.