25.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yajivunia ushiriki wake katika mkutano wa CHOGM

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Serikali imesema kuwa ushiriki wake katika Mkutano wa 26 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya ya Madola (CHOGM) uliofanyika Kigali, Rwanda Juni 19 hadi 25, mwaka huu, umekuwa na mafanikio makubwa.

Hayo yamebainishwa Dar es Salaam leo Jumatano Juni 29, 2022 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula wakati akizungumzia mafanikio ya mkutano huo.

“Kama mnavyofahamu, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni mwanachama hai wa Jumuiya ya Madola toka nchi yetu ilipopata uhuru mwaka 1961 na imeendelea kuwa mwanachama baada ya Muungano mwaka 1964. Kufuatia uanachama huo, Tanzania imekuwa ikinufaika na kushiriki shughuli zote za Jumuiya hiyo. Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Makamu wa Rais Dk. Philip Isdor Mpango ambaye alimwakilisha, Rais Samia Suluhu Hassan.

“Mkutano huu wa 26 umefanyika baada ya kuahirishwa mara mbili (2020 na 2021) kutokana na janga la UVIKO-19 ambalo linaendelea kuitesa dunia hadi sasa. Mojawapo ya mijadala ya mkutano huu ilikuwa ni namna gani dunia itakavyoweza kujikwamua kiuchumi na kijamii kutokana na janga hili,” amesema Balozi Mulamula.

Amefafanua zaidi kuwa mkutano huo wa 26 ulihudhuriwa na Wakuu wa Serikali 27 kati ya nchi 54, ambapo wakuu wengine wa serikali wapatao 27 waliwakilishwa, ukiwa na kaulimbiu, “Delivering a Common Future: Connecting, Innovating and Transforming” ambayo ilijikita kwenye maeneo makuu ya kipaumbele ya utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu; vijana; afya; teknolojia na uvumbuzi; na uendelevu kwenye masuala ya uchumi, biashara, kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na utunzaji wa mazingira.

“Ukichunguza vizuri maeneo hayo ya vipaumbele yanalingana kabisa na vipaumbele vya Serikali ya awamu ya sita, kitu ambacho kilitusukuma kushiriki kwa nguvu kubwa katika mkutano huu. Ikumbukwe kuwa CHOGM 2022 ilitanguliwa na mikutano kadhaa iliyohusisha Majukwaa ya Jumuiya ya Madola; mikutano ya Mawaziri wa Mambo ya Nje, mikutano ya pembezoni (side events) na mikutano ya uwili (bilaterals meetings),” amesema Balozi Mulamula.

Akizungumzia Jukwaa la Biashara, Balozi Mulamula amesema kuwa Ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa la biashara ambalo pamoja na mambo mengine lilijadili fursa za biashara na uwekezaji kwenye Jumuiya ya Madola na Bara la Afrika na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta hizo zikiwemo athari zitokanazo na janga la Uviko-19 na mgogoro kati ya mataifa ya Ukraine na Urusi, uliongozwa na Dk. Hashil Twalib Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara.

“Wajumbe wengine walitoka Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Benki za CRDB na KCB na Chama cha Wakulima wa Maua, Mbogamboga na Matunda (TAHA) na (CTI). Ujumbe wa Tanzania pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji kwenye Jukwaa hili, uliwasilisha kwa wawekezaji orodha ya miradi 115 iliyopo katika sekta mbalimbali nchini kwa ajili ya kutafuta wabia kwenye miradi hiyo kwa utaratibu wa Public Private Partnerships (PPP),” amesema Balozi Mulamula.

Akifafanua kuhusu Jukwaa la Wanawake amesema ujumbe wa Tanzania kwenye Jukwaa la Wanawake (Commonwealth Women’s Forum) uliongozwa na Abeida Rashid Abdallah, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

“Pamoja na ushiriki wa Serikali Asasi mbalimbali za Kiraia kutoka Tanzania nazo zilishiriki. Jukwaa hili lilijadili usawa wa kijinsia na kuwainua wanawake kwenye nyanja zote; kuongeza nafasi za uongozi kwa wanawake; kutoa elimu bora kwa watoto wa kike na namna mabadiliko ya tabianchi yanavyoathiri haki za wanawake.

Jukwaa la Vijana

Amesema vijana saba kutoka Tazania walishiriki Jukwaa la Vijana lililojadili masuala ya ajira kwa vijana, kuendeleza ujuzi na vipaji kwa vijana; elimu kwa vijana; kusaidia vijana wajasiriamali; matumizi ya teknolojia kwa vijana; kujiajiri; na kuongeza udhamini kwenye shughuli za vijana.

“Pia kulikuwa na mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje, walikutana kwenye mikutano miwili: mmoja ulijadili Mkutano wa Wakuu wa Serikali na mwingine ulizungumzia masuala mbalimbali yanayohusu nchi ndogo (small states).

“Kwa upande wa Mkutano wa Mawaziri kuhusu nchi ndogo uliofanyika chini ya Uenyekiti wenza wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda na St. Vincent and Grenadines ulijadili changamoto za nchi ndogo hususan kufuatia janga la UVIKO-19, athari zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi na mgogoro unaoendelea kati ya Urusi na Ukraine pamoja na upatikanaji mdogo wa fedha za maendeleo.

“Baada ya mkutano huo, iliazimiwa kutumia mkakati ujulikanao kama United Nations-Commonwealth Advocacy Strategy, kujenga ubia wa kukabiliana na changamoto zinazokabili nchi ndogo,” amesema Balozi Mulamula.

Ameongeza kuwa, mkutano mwingine wa Mawaziri wa Mambo ya Nje ulijikita kwenye kuandaa mkutano wa Wakuu wa Serikali (Pre-CHOGM Commonwealth Foreign Ministers’ Meeting) kwa kujadili nyaraka mbalimbali za mkutano zilizopokelewa kutoka kwenye mikutano ya Maafisa Waandamizi na mkutano wa watendaji wakuu wa Serikali ambao ulihusisha Makatibu Wakuu-viongozi (Chief Secretaries).

Amesema nyaraka hizo ni: matamko kuhusu usimamizi bora wa matumizi ya ardhi (Commonwealth Living Lands Charter – A Call to Action on Living Lands (CALL)), ukuaji endelevu wa miji (Declaration on Sustainable Urbanization) na huduma na ulinzi kwa watoto (Kigali Declaration on Childcare and Protection Reform) nakuongeza kuwa vikao hivyo vilijadili pia Tamko la Mwisho la Mkutano(Communiqué).

Amesema kuhusu Mkutano wa Wakuu wa Serikali wa Jumuiya ya Madola ulifanyika Juni 24, ulihudhuriwa na Mwana wa Mfalme wa Uingereza, Charles, The Prince of Wales, aliyemwakilisha Malkia Elizabeth II wa Uingereza ambaye ndiye Mkuu wa Jumuiya hiyo; Rais Paul Kagame, Mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Madola kwa kipindi cha mwaka 2022-2024; Boris Johnson, Waziri Mkuu wa Uingereza, aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madola tangu mwaka 2018 na Wakuu wa Serikali wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola walioshiriki CHOGM 2022.

“Baada ya ufunguzi wa Mkutano huo, ulifanyika uchaguzi wa Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola. Wagombea waliojitokeza walikuwa ni Kamina Johnson Smith, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamaica na mgombea kutoka Tuvalu, Sir Iakoba Italeri, ambaye aliingia dakika za mwisho.

“Baada ya uchaguzi huo Patricia Scotland alishinda kwa kupata kura 27 wakati Smith alipata kura 24 na Italeri alipata kura 3.

“Kwa matokeo hayo Scotland anaendelea kuwa Katibu Mkuu wa Jumuiya kwa kipindi cha miaka miwili iliyobaki ya kukamilisha kipindi cha pili cha uongozi wake hadi mwaka 2024,” amesema.

Amesema mada nyingine zilizojadiliwa katika mkutano huo ni pamoja na Utawala Bora na Utawala wa Sheria ambapo waliangalia umuhimu wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Madola kuimarisha demokrasia, utawala bora, na kuheshimu mipaka kati ya mihimili mitatu ya dola ili kufikia mustakabali wenye usawa kwa wote.

“Ajenda hii ni muhimu kwa nchi za Jumuiya ya Madola ikiwemo Tanzania kwa kuwa zinakabiliwa na changamoto katika maeneo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazohitaji misingi mizuri ya demokrasia, amani na utawala bora kupata utatuzi wake.

“Katika mjadala huu, Tanzania ilieleza umuhimu inaotoa kwa kanuni za utawala bora na utawala wa sheria tangu kupata uhuru. Vilevile, Tanzania ilisisitiza umuhimu wa Sekretarieti ya Jumuiya ya Madola kusaidia nchi wanachama kutekeleza programu za kukuza uelewa miongoni mwa watendaji wa taasisi za umma na binafsi ili kutambua majukumu waliyonayo katika kuhudumia wananchi, hivyo kuepuka rushwa na vitendo ambavyo vinakinzana na kanuni za utawala bora na utawala wa sheria,” amesema Balozi Mulamula.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula akizungumza mapema leo Juni 29, 2022.

Amesema mbali na mikutano hiyo pia: “Makamu wa Rais na mimi mwenyewe tulifanya mikutano ya uwili na viongozi mbalimbali waliohudhuria mikutano hiyo. Lengo letu lilikuwa ni kuitangaza nchi pamoja na kuvutia uwekezaji katika sekta mbalimbali zikiwemo za utoaji wa huduma kwa jamii.

“Makamu wa Rais alifanya mazungumzo na Melinda Gates, mwanzilishi mwenza wa taasisi ya Melinda and Bill Gates. Wakati wa mazungumzo hayo, Mhe. Makamu wa Rais aliishukuru taasisi hiyo kwa kuendelea kusaidia Tanzania katika kuboresha sekta ya afya ikiwemo kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza kupitia tafiti na kujengewa uwezo.

“Vilevile, alieleza ukubwa wa changamoto ya malaria nchini Tanzania ambapo alifafanua kuwa zaidi ya asilimia 94 ya wananchi wapo kwenye hatari ya maambukizi ya ugonjwa huo.

“Kadhalika, Makamu wa Rais alifafanua jitihada za kukabiliana na malaria ikiwemo Mkakati wa Taifa wa Mwaka 2021-2025 unaolenga kupunguza maambukizi ya malaria hadi kufikia chini ya asilimia 3.5 ifikapo mwaka 2025 na kutokomeza kabisa ugonjwa huu ifikapo mwaka 2030. Aidha, alieleza upungufu wa bajeti uliopo wa kiasi cha dola za Marekani milioni 540 ili kutekeleza mpango huo kikamilifu,” amesema Balozi Mulamula na kuongeza kuwa:

“Binafsi nilikuwa na mkakati maalum wa kutumia fursa ya mkasinyiko huo wa viongozi kufanya nao mazungumzo. Nilifanikiwa kufanya mazungumzo rasmi na Waziri wa Mambo ya Nje wa Singapore, Dk. Vivian Balakrishnan; Waziri wa Mambo ya Nje wa India, Subrahmanyam Jaishankar; Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, ina Rabbani Khar, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina Mohammed na Mke wa Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza na Mwanzilishi wa Mfuko wa Cherie Blair, Cherie Blair.

“Viongozi Wakuu niliokutana nao sio kwa mazungumzo rasmi, lakini nilifanikiwa kuwapa salamu za Rais Samia ni pamoja na Waziri Mkuu wa Uingereza, Boris Johnson, Waziri, Mkuu wa Canada, Justin Trudeau; Rais wa Rwanda, Paul Kagame; Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema; Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta; na Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari.

“Ujumbe wangu katika mazungumzo hayo ni kuhusu maboresho yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita katika mazingira ya biashara na uwekezaji na kwamba Tanzania ni eneo salama kwa wawekezaji. Maeneo niliyosisitiza ni kilimo, utalii, afya na usafiri wa anga na Uchumi wa buluu hasa katika usimamizi na uendeshaji wa bandari na mafunzo ya teknolojia ya habari na mawasiliano,” amesema Balozi Mulamula.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles