23.8 C
Dar es Salaam
Friday, September 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yajivunia kiwango kikubwa cha Gesi Asilia na mkakati imara wa usambazaji

Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital

Mtaalam wa Visukuku Mimea kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Johanes Kakoki, ameeleza kuwa Tanzania inajivunia kuwa na kiwango kikubwa cha gesi asilia ambacho kinahakikisha upatikanaji wa nishati ya kutosha kwa ajili ya maendeleo ya taifa. Kakoki ameyasema hayo leo Julai 10,2024 wakati wa maonyesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara maarufu Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

Katika maelezo yake, Kakoki alisema kuwa Tanzania ina jumla ya futi za ujazo trilioni 57.54 za gesi asilia zilizogunduliwa. Kati ya hizi, robo tu ya gesi hiyo imetumika hadi sasa, ikionesha kuwa bado kuna akiba kubwa ya gesi ambayo inaweza kutumika kwa miaka mingi ijayo.

“Tanzania imefanikiwa kutumia sehemu ndogo tu ya gesi asilia iliyopo, na hii inatuweka katika nafasi nzuri kwa ajili ya matumizi ya baadaye,” alisema Kakoki. Aliongeza kuwa matumizi haya madogo yanaonesha uwezo wa taifa kujiendesha na kuhifadhi rasilimali hizi kwa maendeleo endelevu ikiwamo kuuza nje ya nchi siku za usoni.

Kakoki alibainisha kuwa TPDC imeweka mkakati imara wa kusambaza gesi asilia kwa wananchi kwa njia ya mabomba na mitandao ya usambazaji ili kuhakikisha kuwa nishati hii muhimu inawafikia Watanzania wengi zaidi. Mkakati huu unalenga kuongeza matumizi ya gesi asilia katika sekta mbalimbali, ikiwemo viwanda, usafirishaji, na matumizi ya nyumbani.

“TPDC inaendelea na juhudi za kusambaza gesi asilia kwa wananchi kupitia miundombinu ya kisasa ya mabomba na mitandao ya usambazaji. Lengo ni kuhakikisha kuwa gesi asilia inapatikana kwa urahisi na inatumika kwa wingi zaidi katika shughuli za kila siku,” alieleza Kakoki.

Aidha, Kakoki alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wananchi katika kufanikisha mpango wa usambazaji wa gesi asilia. Aliwataka wananchi na wadau mbalimbali kushirikiana na TPDC katika kuhakikisha kuwa miradi ya usambazaji gesi inafanikiwa na kuleta manufaa kwa taifa zima.

Mpango wa TPDC pia unajumuisha utoaji wa elimu kwa wananchi kuhusu faida za kutumia gesi asilia kama nishati salama, nafuu na rafiki wa mazingira. Hii ni pamoja na kutoa mafunzo maalum kwa mafundi na watoa huduma wa gesi asilia ili kuhakikisha usalama na ufanisi katika matumizi.

Kwa ujumla, Tanzania iko katika nafasi nzuri ya kuendeleza matumizi ya gesi asilia, ambayo itaongeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kuboresha maisha ya wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles