MWANDISHI WETU
Tanzania, kupitia Wizara ya Viwanda na Bishara na Bohari Kuu ya Dawa (MSD), imeandaa mkakati malumu wa uzalishaji wa dawa, kwa ajili ya kuhudumia nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano wa Mradi wa Uzalishaji Dawa na Vifaa Tiba kwa Ubia wa Sekta ya Umma na Sekta Binafsi jana, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema mchakato huo unaanza wakati Tanzania ikijiandaa kuwa mwenyeji wa mkutano wa SADC, hatua inayoaksi juhudi za Serikali katika kujenga uchumi imara.
Alisema hatua ya ujenzi wa viwanda vitatu vya kutengeneza dawa na vitendanishi nchini itasaidia kunusuru sehemu ya Sh Trilioni 1.2 zinazokwenda nje ya nchi kwa ajili ya ununuzi wa dawa zinazosambazwa nchini na katika nchi za SADC chini ya MSD.
“Kimsingi, wakati Tanzania inakwenda kuwa mwenyeji na kushika uenyekiti wa SADC kuanzia Agosti mwkaa huu, tunahitaji pia kuifanya iwe mzalishaji wa dawa na vitendanishi kwa ajili ya nchi zote 16 wanachama, Afrika Mashariki na Afrika.
“Kwa hiyo tumeweka mazingira rafiki kwa ajili ya uwekezaji mkubwa katika sekta hii ya uzalishaji wa dawa na vitendanishi. Serikali pia inaendelea kupitia sheria ambazo ni kero kwa uwekezaji, ambazo tutazipeleka katika bunge lijalo kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa MSD, Laurean Bwanakunu alisema tayari andiko maalumu kw ajaili ya kuanzisha viwanda vya dawa kwenye maeneo matatu nchini limeshakamilika na sasa wanafanya jitihada za kukaribisha wawekezaji.
Alisema katika wazo hilo jipya la kuanzisha viwanda vya dawa kwa kushirikisha sekta binafsi, ujenzi wa viwanda hivyo vya za hospitali umegawanywa katika maeneo matatu, ambayo ni Mwanza ambapo kutajengwa kiwanda cha bidhaa za pamba, Mbeya kwa ajili ya kiwanda cha maji-tiba na Pwani kwa ajili ya kiwanda cha bidhaa mchanganyiko.
“Kwa sasa MSD ndiyo inayosambaza dawa katika nchi za SADC, lakini asilimia 85 ya dawa zote zinanunuliwa nje ya nchi. Afrika Kusini ndiyo inayoonekana kinara katika nchi hizi kwa mauzo ya dawa, lakini bado ina uhitaji mkubwa kwa sababu inaweza kuhudumia asilimia 25 tu ya watu kwake kwa bidhaa za ndani.
“Kwa hiyo wakati tukielekea katika utani ujao wa SADC, moja ya mambo muhimu ni kuhamaisha uwekezaji wa viwanda hivi vya dawa, ili fedha inayokwenda nje, ambayo kwa sasa inafikia Sh Trilioni 1.2 kwa mwaka ibaki katika nchi hizi,” alisema.
Alisema uwekezaji katika viwanda hivyo nchini utasaidia kupungua gharama za usafirishaji na uhifadhi wa dawa ambazo huchukua hadi miezi tisa kufika nchini, pia utaongeza ajira na kupanua wigo wa teknolojia.
Kamishna wa Ushirikishaji wa Seta ya Umma na Sekta Binafsi (PPP), Dk John Mboya alisema maandiko ya uwekezaji huo utakaogharimu zaidi ya Sh Trilioni 1.1 tayari yameshakamilika, ambapo unatarajiwa kuzalisha zaidi ya ajira rasmi 800.
“Sheria ya PPP pia imeweka wazi kwamba uwekezaji wowote lazima ushirikishe wazawa, kwa hiyo mwekezaji yeyote atakayejitokeza kama akipatikana kutoka nje, atalazimika kushirikisha pia wazawa,” alisema.
Akitoa ufafanuzi, Meneja wa Mradi huo wa Uwekezaji katika Viwanda vya Dawa kwa ubia na PPP, Fred Pondamali alisema hatua ya kupata wawekezaji hadi kusaini mikataba rasmi inatarajiwa kuchukua muda wa miezi sita, hivyo wawekezaji wanatarajiwa kuingia rasmi kwenye ujenzi kuanzia Juni 2020.
“Miradi hii inashindanishwa na watakaoshinda ni wale wenye uwezo wa kifedha na teknolojia. Kwa hiyo utaratibu wa kuwashindanisha hadi kuwakabidhi washindi maeneo ya uwekezaji utachukua muda mrefi kidogo,” alisema.
Alisema katika uwekezaji huo, kiwanda cha bidhaa za hospitali zinazotokana na pamba kinachotarajiwa kujengwa Mwanza kitazalisha bidhaa za aina tatu, cha bidhaa za maji-tiba huko Mbeya kitazalisha bidhaa za aina 10 na cha dawa mseto huko Pwani kitazalisha bidhaa za aina 223.