MWANDISHI WETU
TANZANIA imeshindwa kupata medali katika Mbio za Nyika za Dunia zilizofanyika Machi 30, 2019 Aarhus, Denmark.
Timu mchanganyiko (wanaume na wanawake) ya kupokezana kijiti iliyoundwa na Yohaba Sulle, Sisilia Panga, Mayselina Mbua na Marco Monko ilimaliza nafasi ya tisa ikitumia dakika 28 na sekunde 48.
Katika mbio hizo, Ethiopia ilichukua medali ya dhahabu kwa kutumia dakika 25:49 ikifuatiwa na Morocco kwa muda wa dakika 26:22 huku mabingwa wa mwaka jana Kenya wakishika nafasi ya tatu sekunde saba baadaye.
Katika mbio za kilomita 10 wanaume, Mganda Joshua Cheptegei alimfunika bingwa wa mwaka jana Mkenya Geoffrey Kamworor aliyemaliza nafasi ya tatu na nafasi ya pili ikimwendea Mganda mwingine, Jacob Kiplimo.
Hellen Obiri wa Kenya aliweka historia ya kuwa mwanariadha wa kwanza kushinda Ubingwa wa Dunia (mita 5,000), Ubingwa wa Ndani (mita 3,000) na Mbio za Nyika za Dunia (kilomita 10) baada ya kushinda medali ya dhahabu akiwazidi Waethiopia Dera Dida na Gidey Letesenbet.