22.8 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania, Uingereza zadhamiria kuimarisha Biashara, Uwekezaji

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Tanzania imeeleza dhamira yake ya kuendelea kuimarisha ushirikiano wake na Serikali ya Uingereza katika sekta za biashara pamoja na uwekezaji.

Dhamira hiyo imeelezwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Stergomena Tax (Mb.) aliposhiriki hafla maalum ya kutawazwa kwa Mfalme Charles III na Malkia Camilla iliyofanyika kwenye Makazi ya Balozi wa Uingereza Jijini Dar es Salaam Mei 11, 2023.

Dk. Tax alisema kuwa Tanzania na Uingereza zinafurahia uhusiano mzuri wa kihistoria na kirafiki uliodumu kwa muda mrefu na kuongeza kuwa kupitia uhusiano huo, Tanzania na Uingereza zimekuwa zikifanya kazi kwa ukaribu katika sekta mbalimbali hususan biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande zote.

“Uingereza ni miongoni mwa washirika wa kibiashara wa Tanzania wa siku nyingi na imesalia kuwa miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa kuwa na uwekezaji mkubwa wa Kigeni hapa nchini katika sekta mbalimbali. Tanzania inaahidi kuendelea kushirikiana na utawala wa Mtukufu Mfalme Charles III katika nyanja mbalimbali,” alisema Waziri Tax.

Alisema Uingereza imeendelea kuwa mwekezaji mkuu wa pili nchini Tanzania, ikiwa na jumla ya miradi 956 yenye thamani ya pauni bilioni 4.6 na kuajiri zaidi ya watu 275,000 na hivyo kutoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi.

“Uingereza imeendelea kuwa mwekezaji mkuu wa pili nchini Tanzania, ikiwa na jumla ya miradi 956 yenye thamani ya pauni bilioni 4.6 na kuajiri zaidi ya watu 275,000 na hivyo kutoa mchango mkubwa katika maendeleo yetu ya kijamii na kiuchumi, Tanzania itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Uingereza kwa manufaa mapana ya nchi na watu wake,” aliongeza Dk. Tax.

Dk. Tax alitumia fursa hiyo kuwahakikishia Waingereza na wageni mbalimbali walioshiriki hafla hiyo kuwa, Tanzania ina mazingira salama ya uwekezaji na biashara kwa kuzingatia juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan katika kuboresha mazingira ya uwekezaji na biashara ikiwemo kuweka sera imara na zinazotabirika pamoja na sheria na taratibu rafiki, kuboresha huduma za kijamii, kuimarisha demokrasia, usawa wa kijinsia na utawala wa sheria, kuendeleza miradi mikubwa ikiwemo ya nishati na miundombinu, uchukuzi na usafirishaji.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini, David Concar.

Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini, David Concar alisema Uingereza na Tanzania zimeendelea kuwa na urafiki imara kwa muda mrefu kutokana na heshima, dhamira ya kukuza maendeleo na kuthaminiana kwa wananchi wa pande zote mbili.

“Uingereza imekuwa ikishirikiana na Tanzania katika sekta ya biashara na uwekezaji ambapo wafanyabiashara wengi kutoka Uingereza wamewekeza nchini Tanzania, tutaendelea kuwaeleza kuwa Tanzania ni salama kwa uwekezaji na biashara ili wawekeze kwa wingi,” alisema Balozi Concar.

Balozi Concar aliongeza kuwa Ushirikiano wa Uingereza na Tanzania umekuwa ukistawishwa na juhudi za maendeleo katika sekta mbalimbali hususan za fedha zikiwemo Benki ya Dunia na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

“Uingereza na Tanzania hivi karibuni zitasaini mkataba wa ushirikiano katika sekta ya afya hususan Utafiti wa matibabu lengo likiwa ni kuimarisha sekta ya afya. Uingereza na Tanzania zimekuwa na ushirikiano wa maendeleo kwa lengo la kuendeleza malengo ya pamoja kwa maslahi ya pande zote mbili,” aliongeza Balozi Concar.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles