25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

TANZANIA PRISONS MSIMU UJAO NI KIJESHI JESHI

Na THERESIA GASPER

TANZANIA Prisons ni miongoni mwa timu kongwe katika Ligi Kuu Tanzania Bara, ikifahamika kwa kumudu ushindani dhidi ya vigogo Yanga na Simba.

Makao makuu ya klabu hii inayomilikiwa na Jeshi la Magereza Tanzania yapo katika Jiji la Mbeya.

Prisons ilimaliza msimu uliopita wa Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa kwenye nafasi ya nane.

MTANZANIA lilisafiri hadi jijini Mbeya, ambapo likiwa huko likakutana na kufanya mahojiano na uongozi wa timu hiyo kuhusiana na mikakati yako kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

 

MTANZANIA lilifanya mazungumzo na uongozi wa klabu hiyo ikiwa ni Katibu Mkuu, Havintishi Abdallh na Meneja wa timu hiyo, Erasto Ntabahani, ambao walieleza mikakati yao mipya katika kuelekea msimu mpya.

Usajili

Katibu Mkuu wa Prisons, Havintishi Abdallah, anasema msimu ujao wamepanga kuja kivingine kwa  kufanya usajili wa wachezaji ambao ni waajiriwa na Jeshi la Magereza na kuachana na raia wa kawaida.

Alieleza kuwa lengo la kufanya hivyo ni kuhitaji wachezaji wao wawe na nidhamu ya hali ya juu kama taaluma yao ya jeshi hilo inavyoagiza.

“Wachezaji ambao ni raia wa kawaida wengi wao hawana nidhamu kitu ambacho kinachangia timu kufanya vibaya kwenye ligi.

“Pia kuna wachezaji ambao wamemaliza mikataba na viwango vyao vimeshuka, tumeamua kutoendelea nao.

“Msimu ujao tunakuja na sura tofauti kabisa, tumetoa kipaumbele kwa askari magereza ambao wanakuwa na nidhamu ya kijeshi tofauti na raia,” anasema.

Malengo yao msimu ujao

Abdallah anasema klabu yake  imejiwekea malengo makubwa msimu ujao ambayo ni kuhakikisha inamaliza ligi ikiwa kwenye nafasi tano za juu.

“Kwanza kabisa lazima tuhakikishe tunashinda mechi zote ambazo tutacheza nyumbani lakini pia kuhakikisha ugenini hatupotezi, hatutaki tena kuwa daraja la mafanikio ya timu nyingine yoyote,” anasema.

Ratiba ya Ligi Kuu

Abdallah anasema hawana tatizo na ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lakini anatoa tahadhari akiitaka iepuke mabadiliko yasiyo ya lazima kwakuwa yamekuwa yakiwaathiri.

“Kilio cha kila timu inayoshiriki Ligi Kuu Bara ni ratiba, tunaiomba TFF isiiharibu, kwa upande wetu Prisons hatuoni shida na  ratiba hii, lakini kikubwa tunataka isiharibiwe huko mbeleni.

“Unakuta timu ina viporo vitano kitu ambacho si kizuri, ni vema ratiba ikapangwa vizuri ili wote tuweze kucheza kwa usawa.

“Kama timu inaenda kucheza ugenini mfano Kanda ya Ziwa basi ni vizuri ikamaliza mechi zake zote badala ya wiki moja kutakiwa kurudi tena,” anasema.

Udhamini

Abdallah anasema uongozi wa klabu hiyo upo kwenye mazungumzo na baadhi ya kampuni kwa ajili ya kupata udhamini wa kuwasaidia msimu ujao wa Ligi Kuu.

“Suala la udhamini lina changamoto zake, lakini tumejipanga vyema kuhakikisha msimu ujao tunakuwa na mdhamini ambaye atasimamia baadhi ya vitu ndani ya klabu yetu, naamini uwepo wao utakifanya kikosi chetu kuwa bora zaidi.

“Kwa sasa tupo kwenye mazungumzo na kampuni za Coca-cola, Pepsi, GSM na Shanta Gold Mine.

“Kama tutafanikiwa kupata udhamini utatusaidia katika uendeshaji wa klabu, ikiwa ni pamoja na kupata basi la usafiri kwa wachezaji,” anasema.

“Hadi sasa kuna baadhi ya makampuni ambayo tumefanya nayo mazungumzo nao kama Coca-cola, Pepsi, Saruji, GSM na Shanta Gold Mine tunaozungumza nao,” alimaliza Havintishi.

Benchi la ufundi

Abdallah anasema klabu yake haina desturi ya kubadilisha makocha mara kwa mara na inapotokea chanzo huwa si wao.

“Sisi tunaishi vizuri na makocha kwani tunawapatia kila wanachohitaji na kuhusu suala la kubadilisha mara kwa mara hilo halipo, lakini inatokea wameondoka wanaamua wenyewe,” anasema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles