Na Aziza Masoud, Dar es Salaam
ZAIDI ya nchi 25 zinakutana nchini katika mkutano wa Jukwaa la Vitambulisho vya Elektroniki Afrika unaotarajia kuanza Dar es Salaam leo.
Mkutano huo pamoja na mambo mengine utajadili changamoto zilizopo katika masuala ya uandikishaji na kutafuta njia za kuzitatua.
Mkutano huo wa kwanza kufanyika katika Afrika unatarajiwa kufunguliwa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mathias Chikawe na kuhudhuriwa na zaidi ya washiriki 300 kutoka nje ya nchi.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA), Dickson Maimu, Mkurugenzi wa Mfumo wa Kompyuta, Joseph Makani, alisema mkutano huo wa siku tatu utahusisha nchi ambazo zinatumia Mfumo wa Vitambulisho vya Taifa.
“Kutakuwa na watoa mada kuhusu vitambulisho kutoka nchi mbalimbali duniani ambao wataeleza uzoefu wao katika mataifa wanayotoka. Kila nchi ina changamoto zake kutokana na inavyojiendesha… kupitia mkutano huu tutabadilishana mawazo na kushaurina jinsi ya kukabiliana nazo,”alisema Makani.
Alisema mkutano pia utaisaidia Tanzania kujua nchi wanazotumia Vitambulisho vya Taifa kwa sasa wamefika wapi katika uchumi na wamefaidika nini baada ya kuvitumia katika kutolea huduma mbalimbali za taifa na jamii.
Nchi zitakazoshiriki ni pamoja na Ghana, Rwanda, Botswana, Burundi, Malawi, Zambia, Uganda, Kenya, Djibout, Namibia, India, Mali, Estonia, Zimbabwe, Magascar na Liberia.