Na Derick Milton, Maswa
Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mashimba Ndaki amesema kuwa wizara yake kupitia Wakala wa maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA), ipo katika hatua za mwisho kuhakikisha idadi ya chanjo za mifugo mbalimbali zinazozalishwa nchini zinafika tisa.
Ndaki amesema kuwa kwa sasa Wakala huyo anazalisha chanzo sita kati ya 13 ambazo zinaitajika, ambapo amesema serikali imekuwa ikiagiza chanzo saba kutoka nje ya sita.
Waziri huyo amesema hayo leo Ijumaa Julai 2, 2021 katika Kijiji cha Sangamwalugesha kilichopo halmashuari ya Wilaya ya Maswa, wakati Mwenge wa maalum wa Uhuru ulipowasili kijiji hapo na kuzindua kampeini ya kudhibiti magonjwa ya mifugo katika Wilaya hiyo.
“Kwa sasa Wakala wa Veterinari anazalisha chanjo sita, lakini tuko mbioni kuaza kuzalisha nyingine tatu ili tifikie chanzo tisa, na zile nyingine nne tutaendelea kuagiza kutoka nje ya nchi,” amesema Waziri.
Ameongeza kuwa hatua hiyo ya kuongeza uzalishaji wa chanjo nchini, itasaidia kupatikana haraka na kwa wakati chanjo mbalimbali zinazohitajika kwa wafugaji huku akiwataka kutumia fursa hiyo kuhakikisha mifugo yao inachanjwa kila wakati.
“Tatizo kubwa wafugaji wetu hawana mazoea ya kuchanja mifugo yao mara kwa mara, wanasubilia mpaka wapate tatizo, niwahimize kupitia kampeini hii ambayo imezinduliwa leo wajitokeze kwa wingi kuchanja mifugo yao,” amesema Waziri.
Akisoma taarifa mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge, Kaimu Ofisa Mifugo na Uvuvi Halmashauri Dk. James Kawamala amesema kuwa katika kampeini hiyo halmashuari imejipanga kuanza na zoezi la kuchanja kuku dhidi ya ugonjwa wa kideri au ndondo.
Amese kuwa zaidi ya Kuku Milioni moja katika Wilaya nzima wanatarajiwa kuchanjwa dhidi ya ugonjwa huo, ambao ameeleza umeendelea kusababisha vifo vya kuku wengi katika halmashauri hiyo na kuleta hasara kwa wafugaji.
“Kupitia chanjo hii tunatarajia kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya kuku ambavyo vimekuwa vikisababishwa na kideri, lakini pia kuongeza idadi ya kuku na mayai wenye afya bora pamoja na kuongeza idadi ya kuku na kipato kwa wafugaji,” amesema Dk. Kawamala.
Baadhi ya wananchi wameipongeza serikali kwa kuleta chanjo dhidi ya kuku, ambapo wameeleza wamekuwa wakiangaika na ugonjwa huo dhidi ya kuku wao huku wengi wakipata hasara baada ya kufa.
“Tunaishukuru sana serikali, hii chanjo itatusaidia sana, tumeteseka sana na kuku wetu dhidi ya ugonjwa huu, kuku wamekuwa wakifa mara kwa mara na gafla kutokana na ugonjwa huu,” amesema Masuka Ndala.