21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania kuvuna Sh bilioni 900 za MCC-2

unnamed (18)Washington, Marekani

 

TANZANIA imetimiza masharti yote ya kupatiwa fedha za maendeleo kwa awamu ya pili kutoka Shirika la Maendeleo la Millennium Challenge Corporation (MCC) la Marekani.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Dar es Salaam jana ilisema kutokana na hali hiyo, Tanzania itaanza kunufaika tena na mabilioni ya fedha baada ya wajumbe wa bodi ya MCC kupiga kura ya kuidhinisha kutolewa kwa fedha hizo chini ya Mpango wa MCC-2.

Makubaliano hayo, yamefikiwa wiki iliyopita, kati ya Rais Jakaya Kikwete na Mtendaji Mkuu wa MCC, Dana J. Hyde mjini New York, Marekani.

Mkutano huo pia ulishirikisha watumishi waandamizi wa MCC, akiwamo  Makamu wa Rais wa Operesheni za MCC, Kamran Khan.

“Hongera Rais Kikwete kwa sababu Tanzania imetimiza masharti yote ya kupata fedha nyingine chini ya mpango wa MCC – 2, ikiwa ni pamoja na uongozi wa MCC kuridhika  na hatua za dhati za kupambana na rushwa,” alisema Hyde.

Hyde, alisema bodi ya MCC katika mkutano wake Septemba  mwaka huu na chini ya Mwenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry, imeafiki kuhusu kipengele pekee kilichokuwa kimebakia katika masharti ya kupata fedha hizo.

Alisema kipengele hicho ni kile kinachotaka Tanzania kukabiliana ipasavyo na vitendo vya rushwa.

Tofauti na fedha nyingi zinazotolewa na wafadhili wengi duniani, fedha za MCC hazitakiwi kurudishwa na nchi inayopewa.

Miongoni mwa wajumbe wengine wa bodi ya MCC ni pamoja na Waziri wa Fedha wa Marekani ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bodi, mwakilishi wa biashara wa Marekani duniani na  Mwendeshaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (USAID).

Chini ya mpango huo, Tanzania itapatiwa Dola za Marekani milioni 472.8 (sawa na Sh bilioni 992.80). Kwa kutilia maanani kiasi cha dola milioni 698 (sawa na Sh trilioni 1.46) ambazo zilitolewa chini ya MCC-1.

Fedha zilizotolewa chini ya MCC -1 zilitumika kujenga barabara za Tunduma-Sumbawanga, Tanga-Horohoro na Namtumbo-Songea-Mbinga.

Kwa upande wake Balozi wa Marekani hapa nchini, Mark Childress alisema amefurahishwa na hatua ya Tanzania kukamilisha mchakato wa mkataba mpya.

“Pamoja na Tanzania kufaulu kigezo kilichohitajika, jitihada zaidi za kukabiliana na rushwa ni muhimu ili kuhakikisha utekelezaji na ufanisi wa mkataba huo,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles