*Kupata fursa lukuki, dira ya Rais Samia
Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital
Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Lameck Nchemba amemuahidi Rais wa Benki ya Afrexim kuongeza mtaji wa ziada katika Benki hiyo ambayo Tanzania inamiliki hisa ili iwe na wigo mpana wa kuendelea kupata rasilimali fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Dk. Nchemba ametoa ahadi hiyo Julai 19, 2022 jijini Dodoma alipokutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Benki ya Afrexim, Prof. Benedict Oramah, ambapo walijadili masuala kadhaa likiwemo fursa zinazotolewa na Benki hiyo.
Dk. Nchemba alisema kuwa Serikali itashirikiana na Benki hiyo ambayo kuanzishwa kwake kulikuwa na lengo la kusaidia utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika nchi za Afrika.
“Tunatekeleza dira ya Mhe Rais Samia Suluhu Hassan ya kuweza kuvutia uwekezaji, kuendeleza maeneo mahususi ya uwekezaji (EPZ) pamoja na upande wa Zanzibar ambayo inakusudiwa kutengeneza ajira nyingi kwa vijana ili pato la mtanzania mmojammoja liongezeke na kuweza kupunguza umasikini,” alieleza Dk. Nchemba.
Aidha, Dk. Nchemba amesema kuwa Tanzania inaahidi kuendelea kufanyakazi pamoja na ofisi ya Rais huyo kwa kuzishirikisha Wizara zake, ikiwemo ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Wizara ya Kilimo na Afya ili kuweza kutumia fursa zilizobainishwa na Benki hiyo.
Kwa upande wake Rais wa Benki ya Afrexim, Prof. Benedict Oramah, alisema kuwa Benki yake inafursa nyingi zikiwemo za mikopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, afya na viwanda.
Alizitaja fursa nyingine ambazo Tanzania inaweza kuzipata kuwa ni pamoja na kuwezesha Kanda maalum za kiuchumi, kuongeza thamani ya mazao ya kilimo pamoja na uwekezaji katika hisa kupitia taasisi za fedha.