23.8 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania kunufaika na Dola milioni 100 za mfuko wa uwekezaji kutoka Japan

*Ni za kukuza uchumi, ziliahidiwa katika Mkutano wa TICAD 8, Tunisia

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

TANZANIA ni miongoni mwa nchi za Afrika zitakazonufaika na fedha za Mfuko wa Kukuza Uwekezaji barani Afrika kutoka Serikali ya Japan zitakazotolewa kuanzia Machi, 2023.

Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa timu ya Afrika ya KEIZAI DOYUKAI (Japan Association of Corporate Executives), Bw. Mutsuo Iwai wakati akizungumza na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ofisini kwao Marunouchi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo, Japan.

“Ifikapo Desemba mwaka huu, tutazindua kampuni ya kusimamia mfuko huu wa uwekezaji wenye manufaa barani Afrika na utekelezaji utaanza Machi, 2023. Tunataraji ifikapo Machi, 2024 tutakuwa tumetoa kiasi cha dola za Marekani milioni 100 kwa kampuni za vijana wanaochipukia ili kuwajengea ubia, kujifunza teknolojia mpya na kubadilishana ujuzi,” amesema.

Amesema fedha hizo za uwekezaji kwenye mitaji (start-ups) zimelenga kukuza biashara ambazo zitatatua changamoto za kijamii zikiwemo sekta za afya, kilimo, nishati na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.

Utolewaji wa fedha hizo ni utekelezaji wa ahadi ya Waziri Mkuu wa Japan, Fumio Kishida aliyoitoa Agosti 27, 2022 wakati akitoa hotuba kwenye Mkutano wa Nane wa Kimataifa wa Wakuu wa Nchi na Serikali unaohusu Maendeleo ya Japan na Afrika (TICAD 8) uliofanyika jijini Tunis, nchini Tunisia.

Waziri Mkuu Kishida alisema Japan imelenga kukuza uwekezaji ambapo safari hii wamelenga kuwainua vijana wanaoanzisha makampuni kwani hatua hiyo itawapa fursa vijana wa Afrika na wa Japan kufanya kazi kwa karibu.

KEIZAI DOYUKAI ni taasisi binafsi iliyoanzishwa Aprili 30, 1946 yenye wanachama wapatao 1,500 ambao ni watendaji wakuu na wamiliki wa makampuni makubwa ya Japan wanaojihusisha na utoaji suluhisho kwa masuala ya kisera yanayohusu maendeleo ya nchi yao na dunia kwa ujumla.

Waziri Mkuu pia alikutana na wawakilishi wa Shirikisho la Wafanyabiashara wa Japan (KEIDANREN) ofisini kwao Otemachi, Chiyoda-ku, jijini Tokyo, ambako Mwenyekiti wa Kamati ya nchi zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, Bw. Hajime Kawamura alimweleza jinsi shirikisho lao linavyojihusisha na miradi ya maji, barabara, nishati, mawasiliano utengezaji wa kemikali na ununuzi wa mazao.

Wawakilishi wa kamati hiyo wanaotoka makampuni ya Sumitomo, Marubeni, Toshiba, Komatsu na Mitsubishi walimweleza Waziri Mkuu nia yao ya kuwekeza kwenye miradi ya nishati ikiwemo uzalishaji wa umeme kwa kutumia jotoardhi, usambazaji wa umeme, usambazaji wa gesi (LPG), huduma za mawasiliano na TEHAMA.

KEIDANREN (Japan Business Federation) jumuiya ya kiuchumi iliyoanzishwa Agosti 16, 1946 yenye wanachama 1,494 ambao ni wawakilishi wa makampuni ya Kijapani, ina vyama 108 vya wenye viwanda na taasisi 47 za kiuchumi kutoka mikoa yote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles