25.3 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

TANZANIA KUANZISHA HATI ZA KUSAFIRIA ZA KIELEKTRONIKI

NORA DAMIAN Na GABRIEL MUSHI

-DAR ES SALAAM

KAMISHNA Jenerali wa Uhamiaji, Dk. Anna Makakala, amesema wapo mbioni kuanzisha hati mpya za kusafiria za kielektroniki ambazo zitakuwa na vigezo vya usalama vya kimataifa.

Alisema uamuzi wa kuanzisha hati hizo, umetokana na makubaliano yaliyopitishwa na wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na usalama.

Akizungumza na MTANZANIA jana katika mahojiano maalumu ofisini kwake Dar es Salaam, Dk. Makakala, alisema hati hizo zijulikanazo kama ‘Passport mtandao’ zitakuwa na kadi zenye taarifa za mhusika.

“Kuna mabadiliko ya kiteknolojia katika dunia na ukiangalia katika nchi zilizoendelea, tayari wenzetu walishaanza muda mrefu.

“Hati hizi ni salama zaidi, zina vigezo vikubwa vya ulinzi na ndani kutakuwa na kadi ambayo ikiingizwa kwenye mashine taarifa zote za mtumiaji zitaonekana. Mtu hawezi kufanya ujanja wowote na akijaribu atakuwa ameiharibu hati,” alisema Dk. Makakala.

Alisema hati hizo zinatarajiwa kuanza kutolewa miaka miwili ijayo na matumizi yake yataenda sambamba na za sasa hadi hapo zilizo kwenye mikono ya watu mbalimbali muda wake utakapoisha.

Akizungumzia ubadilishaji wa hati zinazoisha muda wake, alisema mtu akitaka kwenda kupewa nyingine unafanyika uhakiki upya lengo likiwa ni kujiridhisha.

“Hati ya kusafiria ina uhai wa miaka 10, ukiisha mtu akitaka kupewa nyingine si kwamba hatuna kumbukumbu, lakini kwa ajili ya kujiridhisha huwa tunamtaka mtu alete nyaraka upya.

“Watu wasione kama tunawasumbua, kuna ambao waliwahi kupata hati, lakini baada ya kufanya ‘verification’ (uhakiki) unakuta kuna vitu vingine vilifanyika na mara ya pili unaweza kumshika,” alisema.

Akizungumzia hati za kusafiria zenye hadhi ya kidiplomasia, ambazo zimerejeshwa na waliopoteza sifa ya kuzimilika kwa sababu mbalimbali ikiwamo kustaafu, alisema kwa makao makuu ya ofisi hizo Dar es Salaam pekee, zimerejeshwa zaidi ya 100.

“Mwamko ni mkubwa kwa sababu wengi wanarudisha, kwa jana (juzi) pekee hapa makao makuu zimerejeshwa hati 85 na wengine wamerejesha kupitia ofisi zetu za wilaya na mikoa,” alisema Dk. Makakala.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles