26.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 15, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania, Kenya zajadili ushirikiano Sekta ya Umeme na Gesi

Na Mwandishi Wetu, Dodoma

WAZIRI wa Nishati, January Makamba pamoja na Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Isaac Njenga wamekutana na kufanya mazungumzo kuhusu ushirikiano wa Tanzania na Kenya katika Sekta ya Umeme na Gesi.

Mazungumzo hayo yamefanyika Januari 18, 2023 jijini Dodoma ambapo viongozi hao walizungumzia ushirikiano katika kuendeleza nishati ya Jotoardhi, Jua, Upepo pamoja na mradi ya usafirishaji Gesi, usafirishaji umeme na usambazaji umeme vijijini.

Waziri wa Nishati, January Makamba (kushoto) akimsikiliza Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe.Isaac Njenga (kulia) mara baada ya kufika katika Ofisi za Wizara ya Nishati jijini Dodoma ili kuzungumza masuala yanayohusu ushirikiano wa Tanzania na Kenya katika Sekta ya Gesi na Umeme.

Waziri wa Nishati, January Makamba amemueleza Balozi Njenga kuwa, Tanzania ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Kenya katika Sekta ya Gesi na Umeme kwani nchi hizo tayari zina ushirikiano kwenye sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu ya barabara na anga.

Kuhusu mradi wa usafirishaji Gesi kutoka Tanzania kwenda Kenya, amesema kuwa mradi huo ni wa kipaumbele kwa viongozi Wakuu wa nchi hizo mbili na kwamba tayari timu za majadilino kutoka Kenya na Tanzania zimeshaundwa na zinaendelea na kazi ya kuandaa nyaraka mbalimbali zitakazowezesha mradi huo kusonga mbele.

Aidha, kuhusu ushirikiano kwenye Jotoardhi amesema kuwa, Tanzania imeshaanza kuchukua hatua mbalimbali za kuendeleza vyanzo hivyo ikiwemo za upatikanaji wa fedha kutoka vyanzo vya ndani na nje ya nchi na kwamba mtambo wa uchorongaji visima vya jotoardhi kwa ajili ya kuendeleza Jotoardhi unatarajiwa kuwasili nchini mwezi wa Pili mwaka 2023.

Vilevile, amesema Tanzania ipo tayari kushirikiana na Kenya katika kuendeleza vyanzo vya umeme jadidifu vikiwemo Jua na Upepo.

Kuhusu ushirikiano katika miradi ya umeme vijijini, amesema kuwa, ushirikiano huo ni muhimu kwani Tanzania na Kenya zitaweza kubadilishana uzoefu, na hivyo kuweza kufikisha huduma ya umeme vijijini kwa ufanisi zaidi.

Kwa upande wake, Balozi wa Kenya nchini Tanzania, amemueleza Waziri wa Nishati kuhusu nia ya nchi hiyo kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa nishati ya Jotoardhi kwani Tanzania ina vyanzo vya kutosha kuweza kuzalisha umeme kwa kutumia Jotoardhi.

Amesema kuwa, Kenya tayari imeshapiga hatua katika uendelezaji wa Jotoardhi kwani kwa sasa wanazalisha takribani megawati 986 za umeme kwa kutumia nishati hiyo ambayo ni asilimia 46 ya umeme wote unaozalishwa nchini Kenya.

Aidha, Balozi Njenga amemueleza Waziri wa Nishati kuhusu utayari wa Kenya katika kutekeleza makubaliano ya ushirikiano yaliyoingiwa kati ya nchi hizo mbili kwenye mradi wa usafirishaji gesi kutoka Tanzania na miradi ya usafirishaji wa umeme kwa msongo wa kV 400 ambayo itawezesha nchi hizo mbili kuweza kuuziana umeme.

Vilevile, amemueleza Waziri wa Nishati kuhusu Kenya na Tanzania kushirikiana katika miradi ya usambazaji umeme vijijini hali itakayowezesha kila nchi kujifunza mbinu za mafanikio ya usambazaji umeme vijijini.

Kwa upande wa Serikali ya Tanzania, kikao hicho kilihudhuriwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga na Kaimu Kamishna Msaidizi wa Gesi, Mhandisi Joyce Kisamo

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles