33.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi wa Umeme wa Julius Nyerere wafikia asilimia 80.2

Na Mwandishi Wetu,Mtanzania Digital

NAIBU Waziri wa Nishati, Wakili Stephen Byabato, amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) utakaozalisha umeme wa kiasi cha megawati 2,115  umefikia asilimia 80.2.

Naibu Waziri Byabato ameyasema hayo Januari 17, 2023, wakati Wizara ya Nishati ikitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi huo kwa Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini jijini Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe.Dunstan Kitandula (mbele, kushoto) akizungumza baada ya Wizara ya Nishati kutoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere (JNHPP) kwa Wajumbe wa Kamati hiyo jijini Dodoma.

“Kwa sasa utekelezaji wa mradi unaenda kwa kasi  ambapo hadi kufikia Desemba 31, 2022 umefikia asilimia 80.22, aidha mnamo Desemba 22, 2022 zoezi la kuanza kujaza maji katika bwawa la JNHPP lilifanyika kwa kufunga mageti ya njia ya mchepusho,” amesema Byabato.

Kuhusu kazi ya ujazaji maji katika Bwawa la JNHPP amesema kuwa, hadi kufikia Januari 16, 2023 kimo cha maji cha Bwawa kilifikia mita 112.48 kutoka usawa wa bahari kutokea kimo cha mita 74 Desemba 22, 2022.

Naibu Waziri ameongeza kuwa, utekelezaji wa mradi wa JNHPP unaenda sanjari na  utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 400 kutoka eneo la mradi hadi Chalinze mkoani Pwani  na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Chalinze ambapo kwa ujumla miradi hiyo inaendelea kutekelezwa kwa kasi.

Kuhusu malipo kwa mkandarasi wa mradi huo amesema kuwa, tayari Serikali imeshalipa asilimia 74.7 ya malipo hayo ambapo gharama za mradi huo ni shilingi Trilioni 6.5.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Dunstan Kitandula amepongeza Serikali kwa utekelezaji wa mradi huo ikiwemo hatua  ya kuanza kujaza maji kwenye bwawa hilo. Aidha amesisitiza mradi huo kuendelea kutekelezwa kwa kasi ili asilimia za utekelezaji zilizobaki zikamilike kwa wakati.

Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila pamoja na watendaji wengine kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles