Na Ramadhan Hassan,Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Doto James amesema Tanzania imedhamiria kukuza na kuendeleza uwezo wa uzalishaji wenye tija na ufanisi viwandani ili kuongeza ushindani katika soko la ndani, kikanda na kimataifa ili kukuza uchumi na maendeleo endelevu.
James aliyasema hayo, jijini Dodoma Aprili 29, 2021 alipokuwa akifungua kongamano la siku mbili kwa njia ya mtandao linalohusu mikakati oanishi ya kuendeleza uwezo wa uzalishaji viwandani nchini.
Katibu Mkuu aliwasisitiza washiriki kujikita katika kuainisha mikakati oanishi katika sera za viwanda, biashara, uwekezaji na masoko itakayoendeleza njia za uzalishaji mpya na matumizi bora ya njia za uzalishaji zilizopo ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya mwaka 2025 na Malengo ya Maendeleo endelevu.
Aidha, Katibu Mkuu huyo alisema kongamano hilo linafanyika wakati muafaka ambapo mapendekezo yatakayotolewa yatachangia kwa kiasi kikubwa maboresho ya sera zinahusu maendeleo ya Sekta ya Viwanda na Biashara zinazopitiwa na wizara kwa sasa.
Alisema Wizara ya Viwanda na Biashara inatambua hatua mbalimbali zinazotekelezwa na sekta ya uzalishaji katika kukuza uchumi na inaendelea kuchukua hatua mbalimbali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta hiyo ili kuongeza uzalishaji, mauzo ya nje, mazao ya kilimo pamoja kuimarisha uzalishaji wa sekta nyingine.
Pia, aliishukuru UNCTAD na Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizopo nchini kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kutoa msaada wa kitaalamu katika utekelezaji wa miradi mbalimbali katika sekta ya viwanda na biashara hususani Mradi wa Mikakati oanishi wa Kuendeleza Uwezo wa Uzalishaji barani Afrika.
“Tanzania inatekeleza mradi wa mikakati Oanishi wa kuendeleza Uwezo wa uzalishaji Viwandani barani Afrika ili kutathmini uwezo wa uzalishaji, jitihada za maendeleo, changamoto zilizopo na njia sahihi za kuzitatua”.
Kongamano hilo kwa njia ya mtandao, lilihudhuriwa na wawakilishi wa Umoja wa Mataifa, Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP), Shirika Kongamano la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo ya Biashara (UNCTAD), waliopo Tanzania, Geneva na Vienna, Balozi wa kudumu wa Tanzania umoja wa Mataifa Geneva, Watumishi kutoka Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali ya Tanzania bara na Zanzibar pamoja na Sekta Binafsi.
Washiriki hao walipata fursa za kuwasilisha mada mbalimbali na kufanya majadiliano yaliyohusu kuendeleza uwezo wa uzalishaji viwandani na ukuzaji wa sekta binafsi.