Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital
Kampuni ya Tanzakwanza Strategists kwa kushirikiana na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) zimeshauriwa kuanzisha majukwaa ya biashara vijijini ili kuwasaidia wanawake na vijana waliopo huko kuboresha biashara.
Wito huo umetolewa leo Julai 4, jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maluum, Dk. Dorothy Gwajima wakati akifungua jukwaa la wanawake na vijana wafanyabiashara lililoandaliwa na Kampuni ya Tanzakwanza lengo likiwa kuwakutanisha wafanyabiashara wanawake kujadili changamoto zao.
Amesema majukwaa hayo yamekuwa ni muhimu kwani yamekuwa chachu ya maendeleo kwa wanawake na taifa kwa ujumla.
“Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan ndiye kinara katika kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi, hivyo wekeni mpango mzuri wa kuwafikia wanawake waliopo vijijini ili Serikali iweze kuwasaidia Kwani kupitia majukwaa hayo watajitokeza na kujua changamoto zao,” amesema Dk. Gwajima
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wajasiriamali ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa mikopo kwa wanawake na vijana.
Awali, Mkurugenzi Mwenza wa Kampuni hiyo, Francis Daudi ambaye ndiyo waandaji wa jukwaa hilo, amesema wanawake ndiyo kundi kubwa lenye nguvu kiuchumi kuliko makundi yote.
Amesema maendeleo ya kiuchumi yanategemea makundi mawili ambayo ni wanawake na vijana.
Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Biashara TanTrade, Fortunatus Mhambe ametoa wito kwa kampuni hiyo kutanua majukwaa hayo kwa kugusa kila sekta na siyo kuishia kwa sekta nane kama ilivyo sasa kwenye maonyesho hayo.
Jukwaa la Sabasaba Expo Village ni jukwaa la kibunifu linalokutanisha sekta mbalimbali ili kujadili changamoto na kupata ufumbuzi wa changamoto zao.