Na Mwandishi Wetu-Dar es Salaam
MAOFISA watendaji kata 23 katika Manispaa ya Temeke jijini Dar es Salaam, wamepewa mafunzo ya biashara na ujasiriamali kwa lengo la kuhamasisha wananchi katika maeneo yao kutambua fursa zinazowazunguka ili kubadiisha maisha ya wananchi.
Mafunzo hayo yametolewa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kwa lengo la kuwajengea watendaji hao uwezo na mbinu za kuibua fursa za kibiashara.
Akizungumza jana Dar es Salaam kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Temeke, Mchumi wa Manispaa hiyo, Erick Kilangwa, alisema mafunzo yatasaidia wananchi wenye kipato cha kati kuhamasika kuanzisha viwanda vidogo kwa lengo la kwenda na kasi ya Serikali ya Awamu ya Tano yenye dhamira ya kuongeza viwanda.
“Maofisa watendaji kata ndiyo uti wa mgongo wa halmashauri zote nchini kwa sababu ndio wanaokutana na wananchi moja kwa moja, biashara zikishamiri zitaongeza mapato ya halmashauri kwa sababu viwanda ni chanzo kikuu cha mapato katika halamshauri yetu,” alisema.
Alisema Temeke ina viwanda vikubwa 40 na vidogo 158 na kila mwaka Manispaa inakusanya Sh bilioni 18 kutoka kwenye viwanda ambapo kupitia mafunzo hayo, idadi ya viwanda vidogo na vya kati itaongezeke na mapato yataongezeka pia.
Awali akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkurugenzi wa TanTrade, Edwin Rutageruka, alisema mafunzo yalijumuisha masuala mengi ikiwemo namna ya kuandaa mpango wa biashara, namna ya kupata mikopo na changamoto zake, pia washiriki wakaelezwa namna ya kuendeleza uzalishaji katika biashara.
“Kuna bidhaa nyingi zinauzwa bila kufuata utaratibu kama asali ambayo ikiwa itatengenezewa mpango mzuri inaweza kuwa chanzo kizuri cha mapato, vilevile mtajua dhana nzima ya maonyesho ya biashara pamoja na namna ya kushiriki, kila mwaka tumezoea kuona washiriki wengi wakitoka nje, tunataka washiriki watoke hapahapa nchini,” alisema.
Akizungumzia kuhusu wamachinga, Rutageruka alisema: “Hawa wamachinga wanadharaulika lakini wana vipaji vikubwa vya biashara, wanajua namna ya kubadili biashara kulingana na hali ya hewa, wanajua kipindi cha jua kali wauze nini na kipindi cha mvua wauze nini, ni vizuri tukasimishe biashara zao,” alisema