Na WALTER MGULUCHUMA-KATAVI
WAKULIMA Mkoa wa Katavi wamekunwa na hatua ya kuanza kusambazwa kwa tani zaidi ya 900 za mbolea ya mahindi na tumbaku, itakayosaidia kuongeza uzalishaji wa mazao hayo katika mkoa huo.
Wakala mkuu wa kusambaza na kuuza pembejeo, Yara, tayari amefungua ghala kubwa la kuhifadhi mbolea katika Mkoa wa Katavi  lenye uwezo wa kuhifadhi  tani 4,000.
Kaimu Katibu  Tawala wa Mkoa wa Katavi, Crisencia Joseph, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Katavi kwenye uzinduzi wa ghala hilo, alisema mkoa umefarijika kuona mbolea ikiwa imeingia kwa wingi na zaidi tayari imehifadhiwa kwenye ghala  ikisubiri msimu wa kilimo kuanza.
Crisencia alieleza kuwa katika msimu uliopita kulikuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo mbolea kutofika kwa wakati kwa wakulima, baadhi ya mbegu kutoota na wadudu wa kuharibu mazao.
Alitoa wito kwa msimu huu wakulima kuzalisha mazao kwa wingi  kwa kuwa pembejeo zimewahi kuwafikia.
Naye Bwana shamba Mkuu wa Yara, Peter Assey, alisema wao si wanauza mbolea tu bali   wanawekeza katika mnyororo wote wa kuongeza  thamani ya mazao kwa kuanzisha vituo vikubwa vitano katika maeneo ya Moshi, Iringa, Mbeya, Njombe, Morogoro na sasa   Katavi Wilaya ya Mpanda.
Mkurugenzi wa  Wakala Mkuu wa   Yara wa Nyanda za Juu, Olais Oleseenga, alisema hadi sasa jumla ya tani 940 za mbolea  tayari zimeshafikishwa mkoani Katavi huku tani 80 kati ya hizo ni mbolea za tumbaku na tani nyingine ni za mahindi.
Alifafanua kuwa lengo la Yara ni kupeleka tani 4,000 na kuzihifadhi kwenye ghala hilo la Mpanda na tani 2,000 kati ya hizo zitasafirishwa kwenda mkoani Rukwa.
Alisema wamebaini kusafirisha mbolea kwa kupitia Mpanda kwenda  Sumbawanga, gharama zake ni nafuu kuliko kupitia mkoani Mbeya.
Akizungumzia malengo ya mwakani, alisema wanatarajia kupeleka mbolea wilayani  Kasulu mkoani Kigoma kwa kupitia Mpanda kwani kuna usafiri wa kutumia treni hadi Mpanda kutokea Dar es Salaam  na hivyo kufanya bei ya mfuko wa mbolea wa kilo 50 kushuka kwa thamani ya shilingi 4,000 na kumpa nafuu mkulima.