Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
TANI 8,000 za mbolea ya Kampuni ya Yara Tanzania, zimepakuliwa katika Bandari ya Dar es Salaam na kupakiwa katika mabehewa ya Shirika la Reli Tanzania (TRL), kuelekea mikoa ya Tabora na Kigoma.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Petrobena East Africa, Peter Kumalilwa.
Alisema kuondoa mbolea hiyo bandarini na kupelekwa mikoani kunafanywa kwa ushirikiano kati ya kampuni yao na Yara.
“Tunaipongeza Serikali kwa msukumo wake unaotusaidia kuhakikisha mbolea inatoka kwa wakati bandarini ili na sisi tuisafirishe vizuri na iwafikie walengwa kwa wakati,” alisema Kumalilwa.
“Tunafanya hivi kuhakikisha mbolea hii inasafirishwa yote na kuwafikia wakulima mikoani ili kilimo kiwe na tija. Hatutaki tatizo la upungufu wa mbolea lijitokeze katika kipindi hiki,” alisema.
Aliwahakikishia wakulima kwamba udhibiti katika upakuaji na usafirishaji utahakikisha mbolea inawafikia wakulima katika ubora wake na wakulima watanufaika.
Naye Ofisa Operesheni wa Yara Tanzania, Frank Lugoba, alisema kampuni inaendelea kufunga mbolea inayopokelewa katika viwango vinavyotakiwa ili kuiingiza sokoni.