22.6 C
Dar es Salaam
Sunday, July 7, 2024

Contact us: [email protected]

TANESCO yashukuru kwa Kutambuliwa na kupokea Tuzo ya Huduma Bora

Na Esther Mnyika, Mtanzania Digital

Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeelezea furaha na shukrani zake kwa wadau wake kwa kutambua mchango wake katika utoaji wa huduma bora kwa wananchi, hatua ambayo imepelekea shirika hilo kupata tuzo ya mtoa huduma bora. Tuzo hiyo ilitolewa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (DITF).

Akizungumza na Mtanzania Digital Julai 3, 2024, mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Afisa Masoko wa TANESCO Makao Makuu, Innocent Lupenza, alisema tuzo hiyo ina maana kubwa kwao kwani jamii imetambua mchango mkubwa unaotolewa na shirika hilo katika kuhudumia umma.

“Pamoja na changamoto ndogondogo ambazo tunaendelea kuzitatua, tunafurahi kuona mchango wetu umetambuliwa,” alisema Lupenza.

Aliongeza kuwa tuzo hiyo imeongeza morali kwa wafanyakazi wa TANESCO kuendelea kufanya kazi bora na nzuri katika kutoa huduma kwa umma. “Tunashukuru uongozi kwa kutuwezesha kwa yale yote tunayoyahitaji ili kurahisisha huduma bora kwa wateja wetu,” aliongeza.

Lupenza pia alieleza kuhusu huduma ya Jisoti inayotolewa na TANESCO, akisema inamsaidia mwananchi kupata huduma zote na kuripoti changamoto yoyote ya umeme pindi inapojitokeza. “Sasa hivi tumekuja na huduma ya Jisoti ili kumsaidia mteja kupata huduma zetu na kuripoti changamoto ya umeme kwa kutumia simu yake ya mkononi kupitia namba 0748 550 000,” alifafanua.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kutembelea banda la TANESCO lililopo ndani ya viwanja vya maonesho ya Sabasaba ili kupata elimu kuhusu miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika hilo, ukiwemo mradi mkubwa wa bwawa la Mwalimu Nyerere.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles