28.9 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Rais Samia awaita wafanyabiashara kuchangamkia soko huru Afrika

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Rais Samia Suluhu Hassan amewataka wenye bidhaa zenye viwango kwenda katika Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara (Tantrade) na kujisajili ili waweze kunufaika na Soko Huru la Biashara Afrika ambalo Tanzania imeridhia.

Hadi sasa kampuni 11 zimeanza kutumia fursa hiyo muhimu kusafirisha bidhaa za kahawa, katani, viungo, karanga na tumbaku kwenda nchi mbalimbali ikiwemo Algeria, Nigeria, Misri, Ghana na Morocco.

Akizungumza Julai 3,2024 wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), amesema wafanyabiashara wanapaswa kujipanga kuhudumia masoko makubwa ya ndani, kikanda na kimataifa.

“Serikali itaendelea kufanya kila linalowezekana kusikiliza na kutatua changamoto za wafanyabiashara, mfanyabiashara yeyote mwenye maoni ya kuboresha, kujenga na kusaidia nchi milango iko wazi. Waendelee kuwasiliana na mamlaka zetu mbalimbali ikiwemo wizara yenye dhamana ya biashara bila kusahau Tantrade,” amesema Rais Samia.

Aidha amesema wataendelea kujenga, kuboresha na kukamilisha miradi mbalimbali ya miundombinu kuongeza tija ili bidhaa zinazozalishwa zisafirishwe kirahisi kufika kwenye masoko yanayokusudiwa.

Amesema kaulimbiu ya ‘Tanzania ni mahali sahihi kwa biashara na uwekezaji’ ni nyenzo katika kuchochea maendeleo ya ukuaji katika sekta mbalimbali za kiuchumi.

“Tangu maonesho yaanze mwaka 1963 yamejizolea sifa nyingi katika Bara la Afrika na duniani kote, ongezeko la washiriki linaashiria ukuaji wa mvuto ndani na nje ambao umechangiwa na juhudi za serikali katika kusimamia misingi imara na thabiti katika kujenga uchumi jumuishi na shindani kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo biashara, viwanda, uwekezaji,” amesema.

Kulingana na Rais Samia, mwaka 2023 Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilisajili miradi 504 yenye thamani ya Dola za Marekani bilioni 5.68 wakati mauzo ya nje ya bidhaa yalipanda kutoka sh trilioni 12.3 mwaka 2019 hadi Sh trilioni 17.38 mwaka 2023.

“Hii ni kwa sababu watu wanakuja Tanzania, wanaona fursa, wanashiriki maonesho, wanatembelea mabanda na kuona fursa zilizoko Tanzania na kuvutika kuja kuwekeza,” amesema Rais Samia.

Amesema pia uhusiano wa biashara kati ya Tanzania na Msumbiji ulianza karne nyingi kupitia mitandao ya kibiashara iliyochangia kuibuka kwa miji mikubwa ya kibiashara kuanzia Mogadishu kupitia Kilwa hadi Sofala hivyo, ujio wa Rais Nyusi kwenye maonesho hayo unadhihirisha dhamira hiyo.

Ameipongeza Bodi ya Wakurugenzi Tantrade, Mkurugenzi Mkuu, menejimenti na wafanyakazi wote wa mamlaka hiyo kwa juhudi kubwa kuhakikisha maonesho hayo yanafanikiwa.

“Pongezi zangu za dhati kwa mheshimiwa Dk. Ashatu Kijaji ambaye nilimbadilisha kazi jana (Julai 2,2024) kabla ya leo, lakini natambua kazi kubwa aliyoifanya katika kutayarisha maonesho haya na kujenga Wizara ya Biashara na Viwanda,” amesema Rais Samia.

Rais Samia Suluhu Hassan na mgeni wake Rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi, wakitembelea mabanda mbalimbali ya Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba).

Rais Filipe Nyusi ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema maonesho hayo yatumike kukuza fursa za uhusiano ili kuhakikisha kunakuwepo ubia wenye manufaa kwa wawekezaji kutoka Tanzania na Msumbiji.

Amesema uhusiano wa kibiashara baina ya nchi hizo bado hauridhishi ingawa Tanzania ni moja ya nchi zilizowekeza zaidi Msumbiji.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, amesema Tantrade imekuwa ikiratibu maonesho hayo vizuri hatua iliyowezesha kukua mwaka hadi mwaka na kupata washiriki wengi.

Kwa mujibu wa Kigahe, mwaka jana maonesho hayo yalikuwa na washiriki 3,500 lakini kwa mwaka huu wamefikia 3,846.

Mkurugenzi Mkuu wa Tantrade, Latifa Khamis, amesema kupitia maonesho hayo Watanzania wengi wanafaidika kwa kupata ajira ambapo mpaka sasa zaidi ya ajira 17,000 zimepatikana.

“Maonesho yamekuwa ni nyenzo muhimu ya kupunguza uhaba wa Dola za Marekani 433,889 kwa kipindi chote cha maandalizi, ni nyenzo muhimu kwa mapato ya nchi kupitia ukusanywaji wa kodi mbalimbali za Serikali kwa kipindi chote kwani washiriki wote hulipia kodi,” amesema Latifa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles