23.6 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TANESCO YAKABIDHI NYUMBA ZA WALIMU MTERA

Na Mwandishi Wetu -DODOMA

SHIRIKA la Umeme Tanzania, (Tanesco), limekabidhi majengo mawili ya nyumba za walimu kwa Shule ya Sekondari Mtera DAM, iliyoko jirani na Bwawa la kufua umeme wa maji Mtera, (Mtera Hydro Power Plant), lililoko katikati ya mikoa ya Dodoma na Iringa.

Nyumba hizo zilizogharimu Sh milioni 35, moja ikiwa mpya na nyingine imekarabatiwa, zimekabidhiwa kwa uongozi wa Wilaya ya Mpwapwa juzi na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco anayeshughulikia Usambazaji Umeme na Huduma kwa Wateja, Joyce Ngahyoma, kwa niaba ya Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Mhandisi Dk. Tito Mwinuka.

Akizungumza wakati wa kukabidhi nyumba hizo, Ngahyoma alisema wakazi wa Mtera ni wadau na wakubwa wa Tanesco katika kulinda miundombinu ya umeme ya kituo cha kufua umeme cha Mtera ambayo ina gharama kubwa kwa hivyo walipowasilisha maombi ya kujengewa nyumba ya mwalimu mkuu ambapo shirika hilo lilikubali ombi hilo.

“Napenda nichukue fursa hii kuwashukuru wananchi kwa ushirikiano mkubwa mnaotupatia na niwaahidi tu kwamba Shirika litaendelea kushirikiana na Serikali na jamii kwa ujumla katika kuhakikisha sekta ya elimu, afya na huduma nyingine zinaimarika kwa kutoa michango ya hali na mali,” alisema  Ngahyoma.

Alisema pamoja na msada huo, Tanesco imekuwa ikisaidia jamii ya wana-Mtera katika kuwapatia huduma ya afya kwenye zahanati ya wafanyakazi, huduma ya elimu ya awali kwenye shule ya chekechea iliyojengwa kwa ajili ya kuhudumia watoto wa wafanyakazi pamoja na wananchi wanaozunguka eneo hilo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco anayeshughulikia ufuaji umeme, Mhandisi Abdallah Ikwasa, alisema kituo cha kufua umeme wa maji Mtera, kilijengwa mwaka 1984 na kukamilika mwaka 1988 na kuwa na uwezo wa kufua umeme Megawati 80 na tangu kipindi hicho hadi hivi sasa, Tanesco imekuwa ikishirikiana na wananchi katika kulinda miundombinu ya kituo hicho.

Akizungumza katika hafla hiyo ya makabidhiano, Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Jabir Shekimweri, aliwataka wananchi wa Mtera kuendelea kushirikiana na Tanesco, katika kulinda miundombinu ya Shirika hilo kwenye bwawa la kufua umeme wa maji la Mtera.

“Ndugu zangu msada huu umekuja kutokana na faida inayopatikana kutokana na miundombinu hiyo, kwa hivyo niwaombe muendelee kushirikiana na Tanesco na viongozi wa Serikali ya kijiji katika kuhakikisha usalama wa miundombinu hiyo unaendelea kuwepo, kwani wafanyakazi wa Tanesco pekee hawawezi kulinda miundombinu hiyo peke yao kwa sababu eneo ni pana sana,” alisema.

Shekimweri alisema msaada wa majengo hayo utasaidia kutatua changamoto ya nyumba kwa walimu ambao kutokana na uhaba mkubwa wa nyumba walimu wanaishi maeneo ya mbali na shule na hivyo inapelekea utendaji kazi wao kuwa wa chini.

“Nimeambiwa kuwa ufaulu kwenye shule hii ni mzuri na walimu wakiishi maeneo ya karibu na shule, basi ufaulu huo bila shaka utaongezeka sana,” alisema.

Mkuu huyo wa wilaya aliishukuru Tanesco kwa kuisaidia Serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kwenye eneo hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles