Na Sheila Katikula, Mwanza
Shirika la Umeme(TANESCO) Mkoa wa Mwanza linakabiliwa na changamoto ya kukosa njia ya wazi ya kupitisha miundo mbinu ya umeme na kupelekea kukwamisha kasi ya kusambazaji wa nishati hiyo kwa wateja  wao na kusababisha kucheleweshwa kwa maendeleo kwenye baadhi ya maeneo.Â
Hayo yamebainishwa na Mwandisi wa Miradi Mkoa wa Mwanza, Godfrey Vomo alipokuwa akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Mkoa kwenye kikao cha kwanza cha bodi ya barabara ya mkoa wa Mwanza kwa mwaka 2020/2021.
Amesema kuna baadhi ya wajasiriamali kuvamia miundo mbinu ya umeme na kusababisha shirika kushindwa kutekeleza majukumu kwa wakati ya kutoa huduma hiyo.
“Mwaka huu shirika limetenga kiasi cha Sh zaidi ya bilioni 12 kwa ajili ya miradi ya ujenzi wa miundo mbinu mipya na kuboresha na kukarabati pamoja na kuunganisha wateja 17,531. Tunampango wa kuendelea na mpango mkakati wa kuboresha miundo mbinu ya umeme iliyoanzishwa ilikupunguza ukataji wa umeme ifikapo 2021, hivyo tutahakikisha wananchi walipo mjini na pembezoni mwa miji kufikiwa na huduma hiyo,” amesema Mhandisi Vomo.
Amesema vijiji 227 vilikuwa vipate huduma ya umeme kwa kipindi cha mkataba ambao ulifikia kikomo June, mwaka huu, lakini mpaka mwisho wa mkataba mkandarasi hakufanikiwa kuwasha vijiji 80 na havikukamilika hata hivyo serikali kupitia huduma ya umeme vijijini (REA)  waliamua kubadilisha Mkandarasi.