Mwandishi Wetu
Raia 49 wanaoshukiwa kuwa Wahamiaji Haramu kutoka nchini Ethiopia wamekamatwa jana jioni na Askari wa Jeshi la Uhifadhi na Misitu kikosi cha Shirika la Hifadhi za Taifa la Tanzania (TANAPA).
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi – Mawasiliano, Pascal Shelutete amesema kupitia taarifa iliyotolewa leo Jumatano, Novemba 4, kuwa raia hao walikamatwa katika Hifadhi ya Taifa ya Saadani kwa kushirikiana na wananchi katika eneo la Kijiji cha Saadani kando ya Bahari ya Hindi, Bagamoyo mkoani Pwani.
“Uongozi wa Hifadhi ya Saadani, umewakabidhi washukiwa hao kwa Jeshi la Polisi na Idara ya Uhamiaji kwa hatua zaidi za kisheria.
“TANAPA inaendelea kusisitiza na kutoa onyo kwa wale wote wenye dhamira ya kutumia Hifadhi za Taifa kwa vitendo ambavyo ni kinyume na sheria za nchi kuacha mara moja, Jeshi la Uhifadhi na Misitu limejipanga vema kuhakikisha kuwa maeneo ya hifadhi yanaendelea kuwa salama kwa shughuh za Uhifadhi na Utalii na si vinginevyo,” amesema Shelutete.