|Janeth Mushi, Arusha
Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) na Taasisi nyingine za Uhifadhi zimepanga kutumia maonyesho ya Sikukuu ya Wakulima na Wafugaji ya Nane Nane mwaka huu, kutangaza vivutio vya utalii nchini na kupiga vita ujangili.
Hayo yamesemwa na Meneja Kitengo cha Ujirani Mwema kutoka Tanapa, Ahmed Mbugi ambapo pamoja na mambo mengine aliwataja wadau wengine ni Friedkin conservation Fund (FCF) na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro.
Mbugi amesema katika maonesho hayo, Tanapa itatoa magari kuwapeleka watalii hifadhi za taifa za Serengeti kwa washiriki wa maonesho ya kitaifa yanayofanyika mkoani Simiyu.
“Washiriki wa Mkoa wa Morogoro nao watapelekwa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ambapo watachangia gharama kidogo, lengo ni kutangaza utalii na kupiga vita ujangili,” amesema.
Kwa upande wake Naibu Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, Dk. Maurus Msuha, amesema katika maonyesho hayo mbali na elimu mbalimbali juu ya uhifadhi wanayotoa watatumia maonyeshi hayo kupeleka watalii wa ndani kujionea vivutio vilivyopo Ngorongoro.
“Magari maalumu yameandaliwa kutoka Arusha hadi Ngorongoro kutembelea vivutio kwa malipo kidogo,” amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Mwiba Holdings, moja ya kampuni zilizo chini ya FCF, Abdukadir Mohamed amesema katika maonyesho mwaka huu wameandaa mabanda ambayo watayatumia kutatoa elimu ya uhifadhi na vita dhidi ya ujangili.
“Nawaomba Watanzania kutembelea vivutio vya utalii vilivyopo katika mapori ya akiba ambayo yapo katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kukuza pato la taifa,” amesema.