27.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Takwimu mpya homa ya ini tishio

Nora Damian Na Ramadhan -Dar/Dodoma

MGANGA Mkuu wa Jiji la Dar es Salaam, Yudas Ndugile, amewataka wakazi wa jiji hilo kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya ini huku akieleza idadi ya watu ambao wamegundulika kuwa na tatizo hilo kwa kipindi cha miezi sita.

Watu hao ni wale waliokuwa na matatizo mengine ya kiafya, lakini katika vipimo vya kawaida vya maabara wakagundulika kuwa na tatizo hilo pamoja na wachangia damu.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Dk. Ndugile alisema kati ya Januari hadi Juni mwaka huu, watu 5,140 walipimwa kupitia vipimo vya maabara na kati yao 202 sawa na asilimia 3.9 waligundulika kuwa na maambukizi.

Kwa upande wa wachangia damu, kati ya watu 10,084 waliojitokeza kuchangia, 537 sawa na asilimia 5.3 waligundulika kuwa na maambukizi.

“Ukichunguzwa mapema ukabainika kuwa na tatizo, unaweza kutibiwa na kupona kabisa, tatizo ni pale ini linapokuwa limeharibika kabisa,” alisema Dk. Ndugile.

Kuhusu watu waliojitokeza kupima wiki iliyopita wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ugonjwa wa Ini, Dk. Ndugile alisema uchunguzi ulifanyika hospitali tofauti, hivyo takwimu zote zitajumuishwa katika taarifa ya mwezi.

Alisema upimaji wa homa hiyo unafanyika katika vituo vya afya vyenye hadhi ya hospitali na hospitali za rufaa, na kwamba gharama zake ni za kawaida na kuwashauri wananchi kujenga utamaduni wa kwenda kupima.

“Wananchi wameanza kuelewa kwa sababu mahitaji ya watu kuuliza wapi wakapime na kupata tiba yanaongezeka na manispaa ambazo ndio watekelezaji wanaendelea na upimaji na utoaji wa matibabu,” alisema.

Dk. Ndugile pia alitahadharisha watu kuwa makini kutokugusa damu ya mtu mwingine kwa mkono kwani kama ina maambukizi ni rahisi kuambukizwa.

“Magonjwa hayaonekani kwa macho, hivyo hata wale wanaofua nguo za watu waliotoka kujifungua wanatakiwa wavae ‘gloves’ au kuziloweka kwa kutumia dawa ya deto kabla ya kuzifua,” alisema Dk. Ndugile.

DODOMA

Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Benjamini Mkapa mjini Dodoma, Dk. Alphonce Chandika, alisema katika kambi ya uchunguzi iliyofanyika wakati wa maadhimisho hayo, watu 400 walifanyiwa uchunguzi na kati yao 13 walikutwa na maambukizi.

Alisema ugonjwa huo ni hatari kutokana na dalili zake kutokuwa za wazi jambo ambalo linasababisha watu kuchelewa kugundulika.

“Katika kambi ya uchunguzi, kati ya watu 400 waliofanyiwa uchunguzi, 13 wamekutwa na ugonjwa wa homa ya ini, sasa tujiulize kwa ndugu au watu waliohusiana nao huko kabla ya kujulikana, hali zao zikoje na usalama wao ukoje?” alisema Dk. Chandika.

Alisema pamoja na juhudi za Serikali za kutoa chanjo ya ugonjwa huo kwa watoto, lakini bado kuna makundi ambayo yanatakiwa kutazamwa na watumishi wake kupewa chanjo, ikiwa ni pamoja na watoa huduma za afya na polisi.

“Ugonjwa wa homa ya ini unatokana na mtu kugusa majimaji ya mgonjwa aliyeambukizwa kama mate au damu, hivyo kuna makundi ambayo yanatakiwa kupewa msukumo kwa kuwapa chanjo watumishi wake, kama watoa huduma za afya na polisi ambao wamekuwa wakihudumia maiti na majeruhi mbalimbali,” alisema.

WATUMIAJI DAWA ZA KULEVYA

Kamishna kutoka Tume ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Peter Mfisi, alisema watumiaji wa dawa za kulevya, hasa wale wanaotumia njia ya kujidunga na sindano, wako katika hatari kubwa ya kupata homa ya ini ya Virusi B na C.

Alisema takwimu za mwaka 2014 zinaonyesha asilimia 75 ya watumia dawa za kulevya wana virusi aina ya C huku asilimia 80 watu wazima wenye virusi vyenye usugu.

TAKWIMU ZA 2018

Taarifa ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, zilizotolewa hivi karibuni, zinaonyesha wachangiaji damu 13,613 kati ya 307,835 waliojitolea damu mwaka jana, wamebainika kuwa na maambukizi ya virusi vya homa ya ini B.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, vipimo vilivyofanyika kwa watoaji damu 307,835 mwaka jana, vilibaini uwapo wa maambukizi ya virusi vya hepatitis B kwa watu 13,613 sawa na asilimia 4.4 na uwapo wa maambukizi ya hepatitis C kwa watu 1,092 sawa na asilimia 0.35.

Chanjo ya homa ya ini B hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ili kutoa kinga ya muda mrefu na kwa kipindi chote cha maisha yake, na pia chanjo hutolewa kwa watoto na watu wazima walio katika makundi hatarishi ya kupata maambukizi.

Hutolewa katika hospitali za mikoa na vituo vya mipakani na katika hospitali nyingine kama Ocean Road na kwamba utaratibu unaotumika ni kupima kwa Sh 10,000 na kila dozi inagharinu Sh 10,000, hivyo dozi tatu ni Sh 30,000.

MPANGO WA WHO

Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Christine Msanu, alisema ili kuonyesha juhudi zaidi katika kupambana na tatizo hilo, Tanzania ni miongoni mwa nchi kadhaa za Afrika ambazo zitajumuishwa kwenye mpango wa mapambano dhidi ya homa ya ini.

Alisema nchi nyingi ziko nyuma katika uchunguzi na kutibu homa ya ini, hivyo kuna haja ya kuongeza juhudi za mapambano.

Alivitaka viwanda vinavyotengeneza vifaa tiba na dawa kwa ugonjwa huo, kuuza kwa gharama nafuu ili kuwezesha mapambano dhidi ya ugonjwa huo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles