23.1 C
Dar es Salaam
Sunday, September 8, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru yawakalia kooni wakurugenzi Kinondoni, Ubungo

Na Nora Damian, Mtanzania Digital 

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Kinondoni imewataka wakurugenzi wa Manispaa za Ubungo na Kinondoni kuwasilisha katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kodi ya zuio kwa bidhaa na huduma zaidi ya Sh milioni 143.2.

Kodi hizo zilikatwa katika mwaka wa fedha wa 2021/2022 na 2022/2023 na halmashauri hizo lakini hazikuwasilishwa TRA kama inavyotakiwa. 

Akizungumza Novemba 7,2023 wakati wa kutoa taarifa ya utendaji kazi kwa kipindi cha Julai hadi Septemba, Naibu Mkuu wa Takukuru Kinondoni, Elizabeth Mokiwa, amesema walifanya uchambuzi wa mfumo wa ukataji na uwasilishaji wa kodi ya zuio na kubaini dosari hizo. 

“Tulifanya uchambuzi wa mfumo kuhusu ukataji na uwasilishaji wa kodi ya zuio katika ununuzi wa vifaa na huduma katika halmashauri za Manispaa ya Kinondoni na Ubungo, lengo ni kuboresha na kuimarisha matumizi ya risiti za EFD na ukataji kodi ya zuio,” amesema Mokiwa. 

Amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni ilikata kodi ya zuio ya Sh 89,426,979.39 lakini haikuwasilishwa TRA. 

Aidha amesema katika kipindi cha 2021/2022 na 2022/2023 Manispaa ya Ubungo ilikata kodi ya zuio Sh 53,832,188.16 lakini haikuwasilishwa TRA. 

Amesema pia wamefuatilia miradi 11 yenye thamani ya Sh 3,732,846,664 na kutoa maelekezo kwa wahusika. 

Naibu Mkurugenzi huyo amesema pia katika kipindi hicho wamepokea malalamiko 104 na kati ya hayo 59 yalihusu rushwa.

Amesema mashauri mapya mawili yamefunguliwa mahakamani na kufanya kesi zinazoendelea mahakamani kuwa 21. 

Mokiwa amesema wataendelea kutekeleza programu ya Takukuru – Rafiki kwa kuendeleza ushirikiano na wananchi pamoja na wadau wanaohusika na kutoa au kupokea huduma sambamba na wenye jukumu la kusimamia miradi ya maendeleo. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles