22.3 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Mradi wa ReSea wazinduliwa, wananchi Tanga, Pemba kunufaika

Na Faraja Masinde, Tanga

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Waziri Kindamba amezindua mradi wa ReSea unaolenga uhifadhi wa maeneo makubwa ya Bahari kwa ajili ya maendeleo endelevu ya Watu, Hali ya Hewa na Viumbe.

Uzinduzi wa mradi huo wenye thamani ya Dola za Canada milioni 30, umefanyika Novemba 6, 2023 ambapo utanufaisha Mikoa ya Tanga na Pemba kwa Tanzania huku nchi nyingine zikiwa ni Kenya, Msumbiji, Madagascar na Comoro.

Mradi huo wa miaka mitatu unatekelezwa kwa ushirikiano wa Shirika la Mission Inclusion na Shirika la Internation Union for Conservation of Nature (IUCN) kwa msaada wa Serikali ya Canada una lenga kuongeza ustahimilivu wa changamoto za kijamii na kiuchumi kwa watu wanaoishi katika maeneo ya Pwani katika ukanda wa Magharibi ya bahari ya Hindi.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Kindamba amesema wilaya nne zinazonufaika na mradi huo kwa Mkoa wa Tanga ni Mkinga, Pangani, Mheza na Tanga Jiji zikihusisha vijiji 80.

“Bahari kwa watu wa Tanga ni maisha na ni kila kitu, hivyo pamoja na uwepo wa raslimali hizi lakini wananchi wamekuwa wakiitumia kwa kiwango kidogo sana kutokana na ukosefu wa maarifa, hivyo kwa ujio la mradi huu utaenda kuimarisha uchumi wa watu wetu wa Tanga na Pemba kwani tamaduni za watu wetu zinaingiliana.

“Hivyo, uchumi unakwenda kuimarika zaidi na kikubwa nilichofurahi nikwamba mradi huu utahusisha wanawake na vijana takribani 350,000 kwa nchi zote huku Tanzania pekee watu 80,000 wakinufaika, hivyo kila nikiangalia malengo ya mradi huu ni wazi kuwa utawasaidia wananchi kujikwamua kiuchumi na kufanya raslimali za bahari ziendelee kutumika kwa muda mrefu,” amesema Kindamba.

Aonya uharibifu wa mazingira,uvuvi haramu

Amesema jamii inapaswa kutunza mazingira ili kuendelea kuimarisha ustawi wa sasa na baadae.

“Tukomeshe uvuvi haramu, uvuvi wa kutumia mabomu na yote yanayofanyika baharini kwa namna ambayo haikubaliki kwa maslahi ya kizazi kijacho.

“Nitalinda bahari kwa nguvu zangu zote na kwama kuna mtu anataka kunijaribu kwa kucheza na bahari ambayo ndiyo kesho ya watoto wetu basi aharibu bahari.

“Nguvu hiyo hiyo anayoitumia katika kufanya uharibifu, ndiyo hiyohiyo tutakayoitumia kuwadhibiti, Serikali siyo chombo cha kuchekacheka wakati wote bali ni chombo cha mabavu, serikali ni dola, hivyo hatupaswi kucheza na wanaoharibu mazingira ya bahari kwani ni dhambi na nikosa kufanya hivyo,” amesema Kindamba.

Amesema kama mkoa wapo tayari kutoanushikiano kwenye mradi huo kuhakikisha kwamba unafanikiwa na kuleta tija kwa walengwa.

“Tutawapa ushirikiano katika kuhakikisha kuwa mradi huu unafanyikiwa, naomba kuwakumbusha wananchi wa Tanga kuhakikisha kuwa wanatumia mradi huu kwa manufaa ili kujiletea maendeleo, pia niushukuru ubalozi wa Canada kwa mchango wake katika kufanikisha mradi huu ambao ni neema kwa watu wetu, kwani ukiwezesha wanawake umewezesha taifa na dunia kwa ujumla,” amesema Kindamba.

Jinfunzeni Zanzibar

Katika hatua nyingine Kindamba amewahimiza watendaji wa wilaya za mkoa huo kujifunza kwa wenzao wa Zanzibar ambao wameshapia hatua kubwa katika nyanja ya uchumi wa buluu hivyo ni jambo jema kwa watendaji kujifunza.

“Tunajenga nchi moja hivyo ikiwezekana viongozi wa wilaya zetu mwende mkajifunze kwa wenzetu kwani tunajenga nchi moja hivyo hatuna sababu ya kutokujifunza kwa wenzetu waliotangulia, hivyo twendeni Zanzibar tukajifunze kuhusu uchumi wa buluu,” amesema Kindamba.

Awali, Mratibu wa mradi huo wa ReSea, Dorothy Asuza amesema umepangwa kuwa wa miaka mitatu kuanzia Machi 13, mwaka huu na utafikia ukomo Desemba 31, 2025 huku akisisitiza manufaa ya mradi huo.

“Mradi huu unalenga kunufaisha wananchi takwribani 350,000wa jamii ya Pwani, hasa walioathiriwa na mabadiliko ya tabia nchi ndio watakuwa wanufaika wa moja kwa moja wa mradi, sambamba na hilo, watu milioni 2 watanufaika na matokeo ya mradi huu,” amesema.

Upande wake Mkurugenzi wa IUCN Tanzania, Charles Oluchi amesema mazingira ya Bahari na mifumo ya Ikolojia ya Pwani katika ukanda wa Magharibi wa Bahari ya Hindi yanakabiliwa na tishio kubwa kutokana na ukuaji wa mij, ongezeko la idadi ya watu pamoja na mabadiliko ya tabianchi na kwamba mradi huo ni muhimu.

“Mradi huu unakusudia kushughulikia changamoto hizi kwa kuboresha mazingira endelevu ya bahari ambayo yanachangia ustahimilivu wa hali ya hewa na changamoto za kiuchumi za watu wa pwani,” amesema Oluchi.

Balozi wa Canada nchini Tanzania, Kyle Nunas amesema watu wengi zaidi watanufaika na mradi huo zikiwamo jamii za Ukanda wa Pwani katika mikoa ya Tanga na Pemba na kwamba kwa sasa kuna changamoto zinazotokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Canada imejitoa kusaidia mradi huu kuhakikisha kwamba wananchi wanaokaa kwenye ukanda wa bahari wananufaika,” amesema Nunas.

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Agnes Kisaka, mpango huu utasaidia kunyanyua ajenda ya uchumi.

“Tunaishukuru Serikali ya Canada kwa kuwezesha mradi huu kwani, ikumbukwe kuwa mradi huu ni moja ya mikakati ya serikali katika kuhakikisha kwamba inakuza uchumi na kuondoa umaskini kama ailivyoainishwa katika sera ya uchumi wa buluu na nyingine zinazofanana na hizo,” amesema Kisaka.

Uzinduzi huo ulihusisha wadau mbalimbali za mazingira kutoka ndani na nje ya nchi pamoja wawakilishi kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania(JET).

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles