Derick Milton, Simiyu
Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) Mkoa wa Simiyu, imeanza kuzichunguza kampuni 10 kati ya 22 ambazo zilikuwa zikinunua pamba mkoani humo kutokana na kushindwa kulipa madeni ya wakulima.
Mkuu wa Takukuru Mkoa, Joshua Msuya amesema hayo leo Jumanne Januari 21 wakati akizungumza na waandishi wa habari Mjini Bariadi, ambapo amesema kampuni hizo zinadaiwa Sh bilioni 4.5 na wakulima ambapo licha ya kupewa maagizo na viongozi wa kitaifa na mkoa kuhakikisha wanalipa madeni hayo hadi Desemba 31, 2019 lakini wameshindwa.
Kutokana na hali hiyo, Msuya amesema wameamua kuzichunguza kampuni hizo ili kujua ni kwa nini wameshindwa kulipa madeni hayo ya wakulima, ikiwamo kushindwa kutekeleza maagizo ya viongozi.
Hata hivyo, amesema kumekuwepo mkanganyiko wa taarifa za malipo kati ya kampuni hizo na vyama vya msingi vya ushirika (Amcos).
“Kwenye uchunguzi wa awali Amcos zimeleta malalamiko kwetu na kuzitaja hizo kampuni wanazozidai, lakini tuliwaita na kuwahoji kwa nini wanadaiwa, wao walisema tayari wamelipa madeni yao na hawadaiwi,” amesema Msuya.