Ramadhani Hassan -Dodoma
MKURUGENZI Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Brigedia Jenerali John Mbungo amekiri bado kuna changamoto kubwa kukabiliana na rushwa ya ngono vyuo vikuu.
Amesema pamoja na hayo, taasisi hiyo imejipanga kutokomeza jambo hilo, ikiwa ni pamoja na kuwabana wanafunzi ambao wamekuwa wakitoa rushwa ya ngono ili wasaidiwe kufaulu katika mitihani.
Brigedia Jenerali Mbungo alitoa kauli hiyo Dodoma jana, wakati wa warsha ya taasisi hiyo na wadau kujadili matokeo ya utafiti wa rushwa ya ngono katika taasisi za elimu ya juu.
Alisema rushwa ya ngono bado ni tishio kwa jamii, hivyo suala hilo linapaswa kutiliwa mkazo kwa nguvu zote kulikemea.
“Hakuna asiyefahamu rushwa ya ngono inadidimiza utu wa mtu, tushirikiane kuhakikisha suala hili linakwisha kwenye jamii yetu ili kuwaweka wanawake na wasichana katika hali salama,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.
Alisema kutokana na dhamana waliyonayo kusimamia haki kwa kupinga vitendo vya rushwa kwa namna yoyote ile, wamejipanga kushughulikia kero hiyo kwa kuweka madawati ya malalamiko kila mkoa.
Brigedia Jenerali Mbungo alisema madawati hayo yameonyesha kuzaa matunda, mafaili 23 ya kesi yamefunguliwa, huku bado yakiwa yanashughulikiwa kwa kina.
“Jamii itambue rushwa ya ngono ni dhambi, inaangamiza rasilimali za taifa, hatutamwonea haya mtu yeyote atakayejihusisha na vitendo hivi,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.
Mwenyekiti wa Shirika la Ufadhili kwa Wanawake/Wasichana kudai haki zao (WFP), Ruth Meena, alisema pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na Serikali kuwalinda watoto wa kike, bado wanakabiliwa na changamoto ya kupewa vitisho wanapotaka kujinasua katika rushwa ya ngono.
“Wasichana wetu wanapewa vitisho vya kuuawa na wakati mwengine kunyimwa ajira pale wanapotaka kujinasua katika kero hii,” alisema Ruth.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Door of Hope Tanzania, Clemente Mombeki alisema kuwa jamii bado haina uelewa kuhusu madhara ya rushwa ya ngono hali inayokwamisha juhudi za wanaharakati. “Huwezi kujenga taifa kwenye misingi ya rushwa, tuanze kushughulikia hata wale wanaoshawishi,” alisema Mombeki.