Na MWANDISHI WETU-KAGERA
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewataka viongozi wa Takukuru wajiridhishe kama huduma zinatolewa kwa wananchi bila ya rushwa na watakapobaini rushwa wachukue hatua.
Pia amewataka watumishi wa umma wajiepushe na vitendo vya rushwa na matumizi mabaya ya fedha za Serikali katika utendaji kazi wao.
Hayo aliyasema jana wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo katika mkutano uliofanyika katika ukumbi wa JWTZ.
“Msiwalazimishe au kutengenezea mazingira ya kuomba rushwa kwa wananchi. Wananchi mkiona mnazungushwa katika kupatiwa huduma katoeni taarifa Takukuru.
“Tabia ya njoo kesho njoo kesho haikubaliki katika Serikali hii. Serikali haitaki mtumishi mzembe anayedharau wananchi, fanyeni kazi kwa kuzingatia maadili ya taaluma zenu,” alisema Majaliwa
Alisema Rais Dk. John Magufuli alitaka kila Mtanzania afikiwe na huduma za jamii bila ya ubaguzi wa aina yoyote na kwamba mtumshi atakayeshindwa kutekeleza majukumu yake hatakuwa na nafasi serikalini.
Katika hatua nyingine, Majaliwa alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Biharamulo, Wende Ng’ahara awahamishe maofisa kilimo na kuwapeleka vijijini ili wakawahudumie wananchi.
Alisema maofisa kilimo wanaotakiwa kuwepo wilayani ni wawili tu, ofisa kilimo wa wilaya na ofisa kilimo anayeshughulikia mazao ya mbogamboga.
Kadhalika, amemwagiza Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo, Saada Malunde na Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Wende wahakikishe wakuu wa idara wanakwenda vijijini siku nne kwa wiki kuwahudumia wananchi.