JOSEPH HIZA NA MASHIRIKA
UNAPOVINJALI katika maduka makubwa ya kisasa au maduka ya kawaida utakutana na mamia kama si maelfu ya bidhaa iwe vyakula au vitu vya kurahisisha maisha ya binadamu, ambavyo sehemu kubwa ni vya plastiki au vilivyofungashwa au kuwekwa katika plastiki.
Ni kuanzia vyakula kama keki vilivyofungashwa kwa plastiki, mabegi au mifuko ya plastiki kwa ajili ya kuwekea vitu au vyakula, soda zilizo katika chupa za plastiki na sabuni, vibanio vya plastiki na kadhalika.
Kwa binadamu vitu hivi vina thamani kubwa katika maisha yake, vimeyafanya maisha kuwa rahisi na hivyo sehemu ya maisha yake.
Lakini kwa viumbe vya bahari, mazaga zaga haya ya plastiki yanaweza kuwa mabomu yanayoelea majini.
Yaani wakati plastiki vinapoingia katika maji yetu iwe katika mifuko ya plastiki au vinginevyo inatishia viumbe wa baharini, ambao wanaitegemea bahari kwa chakula chao kwa ajili ya uhai na ustawi wao.
Kwa viumbe wa bahari, mifuko ya plastiki inayoelea huonekana kama kiwavi wa baharini na vidonge vidogo vya plastiki—vipande vidogo vigumu vya plastiki, vinavyotokana na bidhaa za plastiki huoneka kama mayai ya samaki kwa ndege wa baharini.
Kabla ya ujio wa kizazi cha plastiki, wakati wavuvi walipotupia baharini taka zao au kupoteza nyavu zao, hazikuwa na madhara.
Hizi zilitengenezwa kwa malighafi asilia kama vile chuma, nguo au karatasi za kawaida ambazo zingezama chini baharini au kubadilika haraka kuendana na mazingira ya eneo la bahari.
Lakini plastiki hubakia vile vile zikielea katika uso wa maji katika eneo lile lile, ambalo vyanzo vya vyakula vingi vya asili kwa ajili ya viumbe bahari hupatikana.
Kumbuka plastiki zina uwezo wa kuelea katika uso huo wa maji kwa miaka 400 kwa sababu uimara wake na hivyo kuhatarisha usalama wa viumbe bahari kutokana na kuvisonga, kuficha vyakula asilia na kadhalika viumbe wanapojikuta wanavimeza huhatarisha maisha yao.
Kwa kukutana navyo wakati wa harakati zao za kusaka chakula, viumbe bahari hushindwa kusonga mbele au kula na kwa kadiri matumizi ya plastiki yanavyoongezeka, ndivyo hatari kwa viumbe bahari inavyoongezeka.
Wakati hali ikiwa hivyo, utafiti umeonesha kuwa iwapo serikali hazitachukua hatua dhidi ya taka hizi za plastiki, ifikapo mwaka 2050, uzito wa taka hizi utazidi samaki.
Kutokana na hatari hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Mpango wa Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP), Erik Solheim ametoa wito kuyataka mataifa kupunguza takataka za plastiki ili kuifanya bahari iwe safi zaidi.
Alisema hayo wakati wa mkutano wa kwanza wa Bahari wa Umoja wa Mataifa uliofanyika mwezi uliopita katika makao makuu ya umoja huo, ambapo uchafuzi wa bahari ni suala linalopewa uzito.
Solheim alikuwa amepokea ombi lililosainiwa na mamilioni ya watu duniani, ambalo linazitaka nchi mbalimbali ziache matumizi ya vitu vya plastiki vinavyotumiwa kwa mara moja tu katika miaka mitano ijayo.
Solheim alisema hivi sasa nchi zaidi ya 20 zimeahidi kupunguza takataka za plastiki, lakini wanahitaji nchi nyingi zaidi kutoa ahadi kama hiyo ili kupunguza takataka zinazoingia baharini kwa kiasi kikubwa.
Takwimu zinaonesha zaidi ya tani milioni nane za takataka za plastiki zinazoingia baharini kila mwaka, zimeathiri vibaya viumbe wa baharini, uvuvi na utalii, na kusababisha hasara ya dola za kimarekani bilioni nane.
Inakadiriwa kuwa takataka za plastiki zinasababisha vifo vya mamilioni ya ndege wa baharini, mamalia 100,000 wa mamalia wa habarini na samaki wengi wasioweza kukadiriwa.
Utafiti unaonesha kuwa kama binadamu hawatachukua hatua kupunguza takataka, ifikapo mwaka 2050, takataka za plastiki zitakuwa nzito zaidi kuliko samaki wote baharini.
Akifungua mkutano huo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres alionya kwamba bahari ziko katika tishio, ambalo halijawahi kuonekana kabla kwa mujibu wa utafiti huo wa karibuni.
Bosi huyo wa UN aliwaambia marais, mawaziri, wanadiplomasia na wanaharakati wa mazingira kutoka karibu nchi 200 kuwa bahari— viumbe wetu wa bahari wanaharibiwa vibaya na uchafuzi wa mazingira, taka na uvuvi mbaya na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Mkutano huo wa siku tano ulianza baada ya Siku ya Kimataifa ya mazingira, ulikuwa tukio la kwanza kujikita katika tabia nchi tangu Rais wa Marekani Donald Trump alipotangaza mwezi huo kuwa Mareani itajiondoa kutoka makubaliano ya Paris ya 2015 ya mabadiliko ya tabia nchi.
Guterres alisema kuwa lengo la mkutano ni ‘kubadili mkondo’ na kutatua matatizo ‘tuliyotengeneza wenyewe.’
Alisema kwamba kulinda maslahi ya taifa na maliasili za eneo husika kunakwamisha maendeleo ya kusafisha na kurudisha afya ya bahari za dunia, ambazo zinachukua theluthi mbili ya sayari yetu ya dunia.
“Tunatakiwa tuweka pembeni maslahi ya muda mfupi ya kitaifa ili kuzuia janga la kipindi kirefu la dunia.
Kuhifadhi bahari zetu na kuzitumia kwa ajili ya uendelevu ili zidumu kwa vizazi vijavyo,” alisema.
Rais wa Mkutano Mkuu wa UN, Peter Thomson, ambaye ni mwanadiplomasia wa Fiji alisema, “wakati umefika kwa mataifa kusahihisha njia ‘zetu’ mbaya.”
“Tumemwaga vya kutosha taka za plastiki baharini ambazo zinanajisi uasili kwa njia nyingi mbaya. Haisameheki kuwa tunamwaga shehena za malori ya taka baharini kila dakika kila siku.”
Alikumbushia ripoti ya mwaka jana ya Jukwaa la Kimataifa la Uchumi iliyosema kuwa kuna tani zaidi ya milioni 150 za taka za plastiki baharini.
“Katika mazingira ya biashara kama kawaida, bahari inatarajia kuwa na tani moja ya plastiki kwa kila tani tatu za samaki ifikapo 2025, na ifikapo 2050, plastiki zitakuwa na uzito mkubwa zaidi kuliko samaki,’ ripot hiyo ilionya.
Aidha ripoti ya mwaka 2014 ya UNEP ilisema uaribifu wa baharini, hasa kupitia taka za plastiki, huathiri kuwepo kwa mikoko na hugharimu zaidi ya dola bilioni 13 kila mwaka.
Ripoti iliyotolewa mbele ya mkutano mkuu wa viongozi na wanasayansi kuhusu utunzaji wa bahari imeonyesha kipindi hicho, ilionesha mikoko huharibika duniani kwa kasi kubwa, mara tano zaidi ya uharibifu wa misitu.
Katika taarifa iliyotolewa siku Septemba 29 ilisema robo ya mikoko iliyopo duniani imeshapotea, kutokana na uchafuzi wa mazingira, kuwepo kwa taka za plastiki baharini, ufugaji wa samaki, kilimo, na mabadiliko ya tabianchi.
Ilipendekeza kuchukuliwa hatua ili kusitisha uharibifu huo, kwani zaidi ya watu milioni 100 hutegemea mikoko kuishi, hasa kwenye nchi zinazoendelea.
Juu ya hayo, mikoko huchangia kwa kiasi kikubwa katika kuzuia kuwepo kwa hewa ya ukaa angani.