27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Taifa Stars kamili kuibeba Tanzania

Na MOHAMED KASSARA-DAR ES SALAAM

KIKOSI cha timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’,  leo kitashuka dimbani kuikabili Senegal, katika mchezo wa kwanza wa fainali za Mataifa Afrika (Afcon) utakaochezwa Uwanja wa June 30, Cairo , Misri.

Stars itatupa karata yake ya kwanza kwenye michuano hiyo dhidi ya Simba hao wa Teranga, ukiwa mchezo wa kundi C, ambalo pia lina timu za Algeria na Kenya.

Baada ya kuivaa Senegal, Stars itashuka dimbani tena Juni 27 kuivaa Kenya (Harambee Stars), katika  mchezo wa pili utakaochezwa Uwanja wa Juni 30, kabla ya kumaliza hatua ya makundi kwa kuvaana na Algeria (Mbweha wa Jagwani) Julai 3.

Kabla ya kuanza mikiki mikiki ya Afcon, Stars ilicheza  michezo miwili ya kujipima nguvu, ikianza kumenyana na Misri  na kupoteza kwa bao 1-0, mchezo uliochezwa Juni 13, Uwanja wa Borg El Arab, Alexandria.

Pia ilijipima na Zimbabwe (The Warriors) na kulazimishwa sare ya bao 1-1, katika mchezo wa pili uliochezwa Juni 16, Uwanja wa El Sekka El Hadid, Cairo .

Senegal kwa upande wao, itaikabili Stars ikitoka kuvuna ushindi wa bao 1-0, katika mchezo wao kujipima nguvu dhidi ya Nigeria uliochezwa Juni 16.

Simba hao wa Teranga watakuwa wanashiriki fainali zao za14 za Afcon, huku mafanikio pekee ambayo hadi sasa wanajivunia ni kufika fainali mwaka 2002 lakini   taji likabebwa na Cameroon.

Stars itacheza fainali hizo kwa mara ya pili, ilishiriki kwa mara ya kwanza mwaka 1980, zilipofanyika nchini Nigeria.

Mara ya mwisho, Stars ilikutana na Senegal Juni 2, 2007, katika mchezo  marudiano wa hatua ya makundi kuwania kufuzu Afcon.

Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Kirumba, Mwanza na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Kiungo Nizar Khalifan ndiyr aliyeindikia Stars bao la kuongoza dakika ya 18, kabla ya Demba Ba kuisawazishia Senegal dakika ya 75.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) limebariki beki wa kulia wa Stars, Hassan Kessy, baada ya kubaini hakuwa na kadi tatu za njano kama ilivyoelezwa awali.

CAF imetoa ruksa hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa nyota huyo alikuwa kadi mbili pekee na si tatu,alizozipata katika michezo miwili ya ugenini ya hatua ya makundi dhidi ya Uganda uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela na kumalizika kwa suluhu, pia na Cape Verde, uliochezwa Praia na Stars kuchapwa mabao 3-0.

CAF ilifafanua kwa kusema, kadi hizo ziliishia mchezo wa marudiano uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na Strs kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde.

Wakati Kocha Mkuu wa Stars, Emmanuel Amunike akishusha presha kutokana na kuwa na uhakika wa kumtumia Kessy, Senegal itamkosa mshambualiaji wao hatari, Sadio Mane ambaye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano.

Mane ambaye ni nyota wa mabingwa wapya wa Ulaya, Liverpool, alipata kadi hizo katika michezo ya hatua ya makundi, hivyo analazimika kukosa mchezo wa kwanza.

Kukosekana kwa Mane aliyemaliza na mabao 22 na kuibuka mfungaji bora wa Ligi Kuu England, inaweza kuwa ahueni kwa Kocha wa Stars Emmanuel Amunike.

Hata hivyo, mabeki wa Stars wakiongozwa na mkongwe, Kelvin Yondani wanatakiwa kuwa makini na mshambuliaji mwingine hatari wa Senegal, M,Baye Diagne.

Diagne anayeichezea Garatasary ya Uturuki, alikuwa moto wa kuotea mbali msimu uliopita, akifunga mabao 30 na kutoa asisti tatu, katika michezo 29 aliyoshuka dimbani.

Licha ya Senegali kuwa na ukuta mgumu unaaongozwa na beki wa Napoli, Kalidou Koulibaly, Amunike atakuwa akijivunia safu yake kali ya ushambuliaji inayoundwa na nahodha,Mbwana Samatta na winga, Simon Msuva.

Samatta akiwa KRC Genk, alimaliza msimu uliopita wa Ligi Daraja la Kwanza A nchini Ubelgiji akifunga mabao 20, huku akitoa pasi tatu zilizozaa mabao katika mechi 28.

Pia aliisaidia Genk kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.

Kwa upande wa Msuva ambaye anakipiga Diffa El Jadida ya Morocco, alimaliza msimu akiwa amepachika mabao 13, pasi nne za mabao katika michezo 24.

Akizungumza jana, katika mkutano na waandishi wa habari, Amunike, alisema amekiandaa kikosi chake kupambana na Senegal.

Alisema anaamini watapata matokeo mazuri katika mchezo huo, kutokana na maandalizi ya kina waliyoyafanya.

Alisema amewaandaa wachezaji wake kucheza na Senegal na siyo Sadio Mane.

“Hata kama Sadio Mane angekuwepo bado tungecheza kama tulivyopanga na siyo kumuangalia yeye peke yake.

“Wachezaji wangu wapo katika hali nzuri, najua tunakutana na timu kubwa, ina wachezaji wazuri, na wapo juu yetu, tutahakikisha tunacheza kwa tahadhari ili tusipoteze mchezo.

Naye Samatta alisema, wamejiandaa vizuri kupambana na kuhakikisha wanaondoka uwanjani wakiwa na matokeo mazuri.

 “Tumejiandaa kikamilifu kwa ajili ya mchezo huo, kila mchezaji ana morali ya juu ya kufanya kitu ili kuipa timu ushindi, tunajua kuwa tuna kazi ngumu, lakini kocha ametupa mbinu za kutosha, tutazitumia kupata matokeo mazuri.

“Tunafahamu Senegal ni timu nzuri na ina wachezaji ambao kila wiki tunakaa na kuwatazama kwenye runinga, hii haina maana tutakaa tuwaangalie wakitufunga, na sisi tutafanya jitihada za kutafuta ushindi,  bila kupambana na timu kama hizi hatuwezi kufikia ubora tunaoutaka, kabla ya fimbili ya kuanza mchezo kupulizwa, kila timu ina nafasi ya kushinda”alisema Samatta.

Kocha Mkuu wa Senegal, Aliou Cisse alisema wanaingia uwanjani wakiwa wanajiamini, lakini wanaiheshimu Tanzania kwakua kila timu iliyofuzu Afcon kutokana na kuwa na kikosi bora,”alisema Cisse ambaye aliwataja Samatta na Msuva katika mkutano huo uliofanyika Uwanja wa Juni 30,akisema ni wachezaji wa kuchungwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles