30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Taifa Stars itaaga kwa heshima AFCON leo?

NA WINFRIDA MTOI

TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo itarusha karata yake ya mwisho, itakaposhuka dimbani kuumana na Algeria, katika mchezo wa hatua ya makundi wa fainali za Mataifa ya Afrika(AFCON) zinazoendelea nchini Misri.

Stars itashuka dimbani  kucheza mchezo wa tatu huku ikiwa tupu, baada ya kupoteza michezo miwili, ikianza kudungwa mabao 2-0 na Senegal kabla ya kutandikwa mabao 3-2 na majirani zao Kenya ‘Harambee Stars’.

Kwa upande wa Algeria,  itaingia uwanjani ikiwa na morali ya juu, baada ya kushinda mechi zake mbili, ikiifumua Kenya mabao 2-0, kisha  kuiliza Senegal bao 1-0.

Mchezo huo utakuwa wa kukamilisha ratiba kwa Stars, kwakua matokeo ya aina yoyote hayataivusha hatua ya 16.

Hiyo inatokana na kupoteza michezo miwili  iliyopita dhidi ya wapinzani wake katika kundi C, Senegal na Kenya huku Algeria  ikiwa tayari  imefuzu kabla ya mchezo wake wa leo.

Kanuni za za mashindano hayo za Shirikisho la Soka Afrika(CAF)zinaeleza kuwa, kama timu  zitalingana pointi, kigezo cha kwanza  kitakachotumika ni kuangalia matokeo ya michezo ya husika zilipokutana.

Ieleweke kwamba, tayari Kenya na Senegal kila moja ina pointi tatu, hivyo hata kama Stars  itaifikia moja wapo bado itakosa kigezo cha kusonga mbele kama timu mshindwa bora(best Looser), ambazo timu nne zinapewa nafasi.

Hata hivyo, Watanzania wanasubiri kuona namna gani kikosi chao kitaondoka Misri, ikiwa ni kwa heshima kwa kupata ushindi dhidi ya Algeria au fedheha kwa kuangusha pointi.

Mara ya mwisho Stars kukutana na Algeria ilikuwa Machi mwaka jana katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliomalizika kwa Algeria kushinda mabao 4-1,Uwanja wa Mustapha Tchaker.

Rekodi za jumla zinaonyesha timu hizo zimekutana mara10, Stars ikishinda mara moja, mabao 2-1 mwaka 1995, ukiwa mchezo wa kufuzu Afcon uliopigwa jijini Dar es Salaam.

Matokeo yanaendelea kusalia vichwani mwa Watanzania wengi, ni kipigo cha mabao 7-0 ilichokipata Stars kutoka kwa Algeria ugenini mwaka 2015.

Akizungumzia Kocha Mkuu wa Stars, Emmanuel Amunike, aliielezea Algeria kama timu imara lakini kwa upande wao  wamejiandaa kupata ushindi.

“Tumecheza na Algeria mara kadhaa, nakumbuka mchezo wa Dar es Salaam  tulifungwa 2-0, baadaye tukatoka nao sare  ya mabao 2-2, pia nakumbuka walikuja kutufunga 7 -0, hiyo yote ni historia.

“Kwa sasa tunaangalia  namna gani tutaweza kusawazisha makosa yetu yaliyotokea katika michezo miwili iliyopita kwa kufanya uamuzi sahihi.

“Jumatatu (leo) tunafungua ukurasa mwingine na ni safari nyingine kwa Tanzania na Algeria, huwezi kutabiri nani atakuwa mshindi, lakini tutaingia uwanjani kupambana na kusaka pointi tatu,” alisema Amunike.

Algeria inaongoza kundi C, ikiwa na pointi sita, ikifuatiwa na Senegal yenye pointi tatu sawa na Kenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles