23.8 C
Dar es Salaam
Friday, July 19, 2024

Contact us: [email protected]

Trump, Kim wakubaliana kuanza tena mazungumzo

SEOUL, KOREA KUSINI

DONALD Trump amekuwa Rais wa kwanza wa Marekani kuingia nchini Korea Kaskazini, baada ya kukutana na Kim Jong-un kwenye eneo linalotenganisha Korea Kaskazini na Kusini.

Nchi hizo mbili zimekubaliana kufufua mazungumzo kuhusu nyukilia yaliyokuwa yamesimama.

Mkutano wao wa mwisho ulivunjika mwezi Februari huku kukiwa hakuna maendeleo yeyote kuhusu mpango wa kusitisha utengenezaji wa silaha za nyukilia.

Wakosoaji wanaona kuwa kukutana kwa viongozi hao kwa mara ya tatu kwa kipindi cha mwaka mmoja kama mchezo wa kisiasa na kusema kuwa Korea Kaskazini bado wanapaswa kuonesha kuwa wamedhamiria kuachana na silaha za nyukilia.

Katika mkutano ambao hatimaye ulipangwa kufanywa baada ya Trump kumwalika Kim kwenye ukurasa wake wa Twitter siku ya Jumamosi, walisalimiana kwa kushikana mikono katika eneo la mpaka kati ya Korea zote mbili kabla ya bwana Trump kuvuka kuingia Korea Kaskazini.

“Ni vyema kukuona tena. Sikutarajia kukutana nawe hapa,” Kim alimwambia Trump huku akitabasamu. Tukio la kukutana kwao lilioneshwa moja kwa moja na televisheni ya kimataifa.

“Ni wakati muhimu,” alisema Trump na kuongeza; “maendeleo makubwa.”

Kukutana kwao mwanzoni ilielezwa kuwa ni kwa muda mfupi, lakini Trump na Kim waliongea kwa takriban saa moja, upande wa Korea Kusini.

Kwa muda mfupi, Trump na Kim waliungana na Rais wa Korea Kusini, Moon Jae-in.

Akizungumza na wanahabari akiwa pembeni ya Trump, Kim alisema mkutano wao ni ishara ya uhusiano wao mzuri sana.

Akiita urafiki wao mzuri, Trump ambaye awali alimuita Kim ‘mtu wa roketi’, akisema ni siku nzuri kwa dunia na kwamba anajivunia kufika kwenye mpaka wa nchi hizi za Korea.

Marais mbalimbali wa Marekani walitembelea eneo la mpaka linalogawanya peninsula tangu kumalizika kwa vita ya Korea mwaka 1953, kuonyesha kuiunga mkono Korea Kusini.

Rais wa zamani wa Marekani, Jimmy Carter na Bill Clinton walishawahi kutembelea Korea Kaskazini, mjini Pyongyang-lakini baada ya kuondoka madarakani.

Trump alionekana kufurahia sana tukio hili la kufika kwenye eneo la mamlaka ya nchi ambayo kwa muda mrefu, imekuwa adui.

Mahusiano haya yamepunguza mzozo kwenye peninsula ya Korea, lakini hayajafanya Korea Kaskazini kusitisha mradi wake wa kutengeneza silaha za nyukilia.

Uhusiano wao umefanya kuwepo kwa tabasamu na kushikana mikono, lakini si kusitishwa kwa utengenezaji wa siaha za nyukilia katika eneo la peninsula ya Korea.

USHAWISHI UNAENDELEA?

Wapatanishi kutoka pande zote mbili watakutana wiki zijazo kuanza mazungumzo kuhusu mradi wa nyukilia wa Korea Kaskazini, Trump amewaambia waandishi wa habari, akisema hatafuti kasi ya kufikia malengo, bali kutekeleza vyema malengo.

Vikwazo dhidi ya Korea Kaskazini, aliongeza kuwa vitaendelea kuwepo ingawa kuna uwezekano wa kupunguza ikiwa sehemu ya mazungumzo.

Trump alisema amemkaribisha Kim kutembelea Washington.

Wachambuzi wa mambo wana shaka kama mkutano huu utazaa matunda hasa kuhusu kukomesha uzalishaji wa silaha za nyukilia.

Huu ni mkutano wa tatu kwa viongozi hao wawili katika kipindi cha mwaka mmoja. Kukutana kwa viongozi hao kumeongeza matumaini ya kuyarejesha mezani mazungumzo ya nyuklia yaliokwama.

Trump aliandamana na Kim kuvuka eneo hilo la mpaka lisilo la kijeshi na ambalo kwa miaka kadhaa limekuwa katika fukuto la Vita Baridi.

Trump aliwasili Korea Kusini juzi jioni kwa ajili ya mazungungumzo na Moon baada ya kuhudhuria mkutano wa kilele wa mataifa 20 yalioendelea kiviwanda duniani huko Osaka, Japan, ambapo alifanya ziara ya kushtukiza na kutoa wito wa kutaka kuonana na Kim na hatimae jambo hilo kufanikiwa.

BBC

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles