30.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 18, 2024

Contact us: [email protected]

TAIFA LINAHITAJI MUDA KUJITAFAKARI KUFIKIA HATIMA TUITAKAYO

maguKUNA tofauti kubwa kati ya taifa na nchi. Taifa ni watu wanaoishi ndani ya mipaka iitwayo nchi. Nchi yetu ina utajiri wa kutisha ila Taifa letu kwa maana ya watu wake walio wengi ni maskini wa kutupwa. Nchi yetu haina shida ya umaskini ila Taifa letu ndio lina tatizo la umaskini.

Taifa letu limepewa jina la nchi ya dunia ya tatu kwa sababu ya kiwango cha umaskini kinachowakabili wananchi wake walio wengi. Nchi yetu ina ukubwa wa eneo la mita za mraba 95,000. Ni nchi kubwa na nchi pana, watu wake hawana budi kujipanga sawasawa ili kuondoa umaskini kwa kila mwananchi. Huu ndio msingi wa makala haya ya juma hili kuwa nadhani imefika wakati kwa watu wa Taifa hili tujitafakari kuwa wanataka kufikia hatima ipi kwa kuwa tunajiendea endea kwa kupapasa bila kuwa na mwelekeo unaoeleweka.

Mataifa yaliyoendelea yalijiwekea uhakikisho wa ustawi wa mataifa yao kwa sababu waliamua kutafsiri dira zao kwa kuwekeza kwenye mambo ya msingi. Moja ya jambo kubwa la msingi la kwanza katika Taifa ni kuendeleza watu wake kielimu. Ni muhimu kuendeleza watu wa nchi fulani kwa sababu  watu ndio Taifa. Hoja hii ndiyo ilimfanya Mwalimu Nyerere aseme kuwa maendeleo si ya vitu, maendeleo ni ya watu. Hatuhitaji kununua vitu ili kuwafurahisha watu, tunapaswa kuwaendeleza watu ili kulifurahisha Taifa. Ukiwaendeleza watu wao wataendeleza vitu! Hivyo hatuna budi kuwaendeleza watu wetu hasa kuwekeza kwa watoto wetu!

Tusirudie makosa tuliyowahi kuyafanya mara baada ya Uhuru. Tulikuwa na maendeleo ya vitu, tulikuwa na viwanda zaidi ya 10 vya nguo ambavyo vyote vilikufa kwa sababu vilikosa watu wenye utaalamu wa kuviendesha kibiashara! Tulikuwa na Shirika la Ndege ambalo lilikufa kwa sababu lilikosa watu makini wa kuliendesha. Tunapoona maendeleo katika mataifa mengine ni ishara kuwa waliwaendeleza watu wao kielimu na sasa wanawatumia kuliendeleza Taifa!

Kila taifa lina watu wenye akili sana kuzidi wengine ambao taifa huwabaini na kuamua kuwatumia kuendeleza watu wa taifa hilo. Njia bora ya kubaini watu wenye vipaji katika akili zao ni kuwaendeleza kupitia mfumo wa elimu unaoweza kubaini vipaji vya kila mtu. Kwa asili kila mtu ana kipaji ambacho kinalifaa taifa, hakuna mtu ambaye hafai katika taifa.

Mfumo wetu wa elimu una njia moja tu ya kupima vipaji vya akili za watu nayo ni mitihani ya darasa la nne, darasa la saba, kidato cha pili, kidato cha nne na kidato cha sita. Hatuwezi kupima vipaji vya akili ya watoto wetu kupitia kipimo kimoja pekee, tunafeli kama Taifa. Shule za ufundi zinaanza baada ya mtu kumaliza darasa la saba au kidato cha nne. Shule za ufundi zinawachukua watoto wale ambao walifeli mitihani yao katika elimu ya msingi na elimu ya sekondari. Hapa tumefeli kama Taifa! Tunashindwa kubaini vipaji vya akili za watoto wetu kwa sababu ya mfumo mbovu wa kubaini vipawa na kuviendeleza!

Tumejisahau na tumebweteka! Hii ndio sababu mwanafunzi wa Chuo Kikuu akimaliza chuo, huenda kufanya kazi tofauti kabisa na mfululizo wa masomo aliyosoma akiwa chuoni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles