25.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Taifa Gesi yagawa mitungi 300 kwa wajasiriamali, Jafo aipa tano

Na Gustafu Haule, Pwani

KAMPUNI ya uuzaji na usambazaji wa gesi nchini ya Taifa Gesi imegawa bure mitungi ya gesi 300 kwa wajasiriamali mbalimbali wakiwemo mama lishe na wadau wengine ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha jamii juu ya utunzaji wa mazingira na matumizi ya nishati mbadala.

Mitungi hiyo imetolewa leo Aprili 20, 2023 katika uzinduzi wa kampeni ya utunzaji mazingira na matumizi ya nishati mbadala uliofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Ruvu iliyopo katika Halmashauri ya Kibaha Vijijini.

Uzinduzi huo umefanyika huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Dk. Selemani Jafo pamoja na viongozi wengine wa Serikali.

Meneja wa mambo ya ushirika kutoka Taifa Gesi, Anjela Bhoke.

Awali, Meneja wa mambo ya ushirika kutoka Taifa Gesi, Anjela Bhoke alisema kuwa mbali na kutoa mitungi hiyo lakini kampuni imeandaa mashindano maalum kwa waandishi wa habari kuhusu kuelimisha jamii athari za ukataji miti hovyo.

Bhoke, amesema Taifa gesi pia imeandaa shindano lingine la kupata Halmashauri bora katika kudhibiti ukataji wa miti hovyo na usafirishaji wa mkaa kutoka Mkoa wa Pwani kwenda Jijini Dar es Salaam.

Amesema athari za ukataji miti hovyo ni kubwa kwani inapelekea kuwepo kwa mabadiliko ya tabia ya nchi hususani kwa ukosefu wa mvua,madhara ya kiafya na hata athari nyingine za kimazingira.

Bhoke amesema Taifa gesi wanaunga mkono jitihada za Serikali ya awamu ya Sita chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan katika kupambana na vitendo viovu vya ukataji miti hovyo ambapo ukadiriwa kuwa ekari 400,000 za misitu zinapotea kila mwaka na hivyo kuleta madhara katika jamii.

“Katika uzinduzi wa kampeni hii Taifa gesi imeandaa mashindano mbalimbali yakiwemo ya waandishi wa habari, mashindano ya kupata Halmashauri bora na hata kutoa bure mitungi ya gesi 300 kwa mamalishe na wadau wengine na tunafanya hivi kwa ajili ya kuunga mkono Serikali yetu dhidi ya vitendo viovu vya ukataji miti hovyo,” amesema Bhoke.

Aidha katika uzinduzi huo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dk. Jafo ameishauri  kampuni ya Taifa gesi kuona uwezekano wa kuingia makubaliano na shule za sekondari pamoja na taasisi za umma ili  kuwafungia mtambo wa gesi katika maeneo yao.

Jafo,amesema makubaliano hayo yatawezesha kampuni na shule za bweni kulipa fedha za kufungiwa mitambo hiyo kidogo kidogo huku wakiendelea kutunza mazingira na kuipunguzia Serikali gharama za uendeshaji wa  Shule hizo.

Jafo, amesema amefurahishwa kuona   mtambo wa Taifa gesi uliofungwa katika shule ya Sekondari ya Wasichana Ruvu kwani unakwenda kupunguza gharama zilizokuwa zinatumiwa na uongozi wa shule hiyo kununua mkaa na kuni.

Kwa mujibu wa Jafo, shule hiyo ilikuwa inatumia kiasi cha sh.milion nne kwa mwezi kwa ajili ya kununua kuni na mkaa lakini baada ya kufungiwa mtambo huo gharama zimeshuka watakuwa mpaka kufikia kiasi cha sh milioni mbili kwa mwezi.

“Naipongeza Kampuni ya Taifa gesi kwa kuanza utekelezaji wa agizo la Serikali la matumizi ya nishati mbadala na nimeona mmefunga mtambo mkubwa wa gesi hapa shuleni ,naomba pelekeni teknolojia hii katika Shule zote lakini anzeni Shule za Pwani,” amesema Dk. Jafo.

Jafo, ameongeza kuwa kati ya mikoa  minne hapa nchini ambayo imeathirika kwa uharibifu wa mazingira mkoa wa Pwani ni mojawapo huku akimpongeza Mkuu wa Mkoa huo Abubakar Kunenge kwa jitihada anazozifanya kusimamia kampeni ya kupanda miti.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mkuu wa Wilaya ya Kibaha Nickson Saimon amesema kutokana na mkoa huo kuwa karibu na Jiji la Dar es Salaam imesababisha kuathiriwa zaidi na uharibifu wa mazingira kwa kuzalisha mkaa mwingi.

Hatahivyo ,Saimon amesema kuwa Mkoa huo tangu umeanzisha kampeni ya kutunza mazingira wamefanikiwa kupanda miti milioni 9.7 sawa na asilimia 25 ya malengo waliojiwekea  lakini wamejipanga vizuri katika utekelezaji wa kampeni hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles