*Watoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kumiliki ardhi kisheria
Na Clara Matimo, Mwanza
Shirika lisilo la Serikali linalojishughulisha kuboresha makazi na uchumi wa nyumbani(TAHEA pamoja na Chama cha wanawake Wanasheria Tanzania(TAWLA) ambao ni wadau wa ardhi wameadhimisha siku ya makazi duniani kwa kupanda jumla ya miti 3,000 katika Wilaya za Ilemela na Misungwi mkoani Mwanza.
Siku ya makazi huadhimishwa duniani kote kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba kila mwaka, lengo likiwa ni kutathmini changamoto zinazoikabili sekta ya nyumba na makazi, hali ya miji midogo na mikubwa, usawa wa kijinsia na malengo ya maendeleo ya kitaifa na kimataifa ambayo taifa limejiwekea katika kukuza uchumi na kutekeleza malengo ya maendeleo endelevu.
Kwa mwaka huu maadhimisho hayo yameongozwa na kauli mbiu isemayo ‘Uchumi thabiti wa mijini, miji kama vichocheo vya ukuaji wa uchumi’.
Akizungumza Oktoba 2, 2023 kwenye maadhimisho hayo, yaliyofanyika Kata ya Kiseke wilayani Ilemela, mkoani Mwanza, Meneja Miradi kutoka Tahea, Mussa Masongo alisema wamepanda miti hiyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa ‘Tufunguke’ unaotekelezwa na Serikali katika halmashauri tano mkoani Mwanza kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ardhi likiwemo shirika lake pamoja na TAWLA.
Amesema mradi huo unagharimu zaidi ya Sh milioni 700 ambao ni ufadhiliwa na Shirika la Kimataifa We Effect la nchini Sweden lenye makao yake makuu jijini Nairobi nchini Kenya.
Masongo amefafanua kwamba kati ya miti hiyo ambayo wameipanda kwenye taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo hospitali na shule ili kuwa na uhakika wa kupata matunzo kama kumwagiliwa maji na ufuatiliaji imo ya mbao, matunda na kivuli, ambapo 2,000 imepandwa wilayani Ilemela na 1,000 Misungwi.
“Leo ni siku ya makazi duniania lengo letu ni kuadhimisha siku hii kwa kuikumbusha jamii kuhusu majukumu na wajibu wao juu ya uhifadhi na utunzaji wa mazingira, kutunza mazingira ni suala mtambuka ambalo kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kushiriki. Kwa mfano, tumesikia mamlaka husika inatangaza uwezekano wa kunyesha mvua za El-nino, wote kwa pamoja tunapaswa kuweka mikakati ya kuzuia makali ya mvua hizo kwa jamii.
“Kila mtu aone thamani ya mti kwa sababu mti unapunguza hewa ya ukaa, unaweka kivuli na unapunguza joto katika maeneo yetu tukikata miti tutakosa mvua ama zitachelewa,” alisema Masongo na kuongeza:
“Tahea inaunga mkono juhudi za serikali kwa kuwahamasisha wananchi kuwa na makazi bora kwa kujenga nyumba bora, utunzaji wa mazingira na uhakika wa chakula, tumekutanika hapa kulingana na lengo namba 11 la dunia lisemalo miji na jamii endelevu ambapo pia linalenga kuhamasisha jamii katika kuwekeza juu ya masuala ya ulinzi, usalama wa chakula upatikanaji wa ardhi iliyopangwa vizuri kwa matumizi bora hivyo tunasisitiza jamii kuepuka ujenzi holela,” amesema Masongo.
Mratibu wa mradi wa ‘Tufunguke’ kutoka Chama cha Wanawake Wwanasheria Tanzania (TAWLA), Wakili Fatuma Kimwaga, aliiasa jamii kujenga katika maeneo ambayo yamepimwa maana ni salama, kufuata taratibu za kumiliki ardhi, kufuata ramani ya mipango miji na kupata hati miliki kwa sababu hati hizo zinaweza kuwasaidia kupata mikopo na kujiinua kiuchumi.
“TAWLA tumekuwa tukitoa elimu juu ya haki ya mwanamke kumiliki ardhi, maana nyenzo ya ulinzi wa haki ya mwanamke kwenye ardhi ni kuwa na nyaraka inayoonyesha umiliki hivyo rai yangu kwa wanawake wenzangu leo hii siku ya makazi duniani tusijenge maeneo ambayo si salama, kama ya shule, msikiti kesho na kesho kutwa unaanza kulalamika ukitaka hamashauri ikulipe fidia pia wanaotengeneza nyaraka mbalimbali za kuhamisha miliki waweze kuandaa nyaraka ambazo zinaweza kuwasaidia wanawake hawa,” alisema Wakili Kimwaga.
Akizindua upandaji miti, Katibu Tawala Wilaya ya Ilemela, Mariam Msengi, aliwapongeza wadau hao kwa kuunga mkono juhudi za serikali kutunza mazingira, kuhamasisha jamii ujenzi wa nyumba bora na usalama wa chkula ambapo alibainisha kwamba wilaya imejiwekea lengo la kupanda miti million moja ndani ya mwaka huu hadi sasa wamekwishapanda 38,035 katika maeneo mbalimbali na mingine inasubiri msimu wa mvua.