27.9 C
Dar es Salaam
Monday, June 24, 2024

Contact us: [email protected]

Taharuki bungeni

Pg 1bElias Msuya, Dodoma na Elizabeth Hombo, Dar

MKUTANO wa Bunge ulivunjwa jana baada ya wabunge wa kambi ya upinzani kupinga kauli ya Serikali kuhusu Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kutotangaza moja kwa moja mikutano ya Bunge.

Kauli hiyo iliyotolewa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye saa 5:50 asubuhi, ilimpa wakati mgumu Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge ambaye alilazimika kukabiliana na wabunge wa upinzani waliopinga tamko la Serikali wakitaka mikutano ya Bunge iendelee kuonyeshwa moja kwa moja na televisheni hiyo ya taifa.

Akitoa kauli hiyo, Nape alisema tangu TBC imeanza kuonyesha vipindi hivyo moja kwa moja, imejikuta ikipata gharama kubwa zinazofikia Sh bilioni 4.2.

“Kabla ya kuanza kurusha moja kwa moja, TBC wakati huo (Televisheni ya Taifa), ilikuwa inarekodi matukio yote na kurusha usiku katika vipindi maalumu vilivyojulikana kama ‘Bungeni Leo’,” alisema Nape na kuongeza:

“Baada ya kuanza kwa utaratibu wa kurusha matangazo moja kwa moja mwaka 2005, gharama za kufanya kazi hiyo zimekuwa zikipanda kwa kasi hadi kufikia Sh bilioni 4.2 kwa mwaka.”

Alisema TBC imekuwa ikigharamia sehemu kubwa ya matangazo hayo kwa kutumia mapato yake yanayotokana na matangazo madogo ya biashara.

“Hivyo basi, TBC imeona ni busara kuanzia mkutano huu wa Bunge iwe inarusha baadhi ya matangazo ya Bunge moja kwa moja ikiwa ni njia ya kubana matumizi,” alisema Nape.

Alisema katika utaratibu huo, TBC itahakikisha baadhi ya matukio ya Bunge yanarushwa moja kwa moja na mengine kurekodiwa na kuandaliwa kipindi maalumu kitakachoitwa ‘Leo katika Bunge’.

Aliongeza kuwa kipindi hicho kilichoanza Januari 26, mwaka huu kitakuwa kikirushwa kuanzia saa nne hadi saa tano usiku, huku akidai kuwa baadhi ya wananchi wameanza kuridhishwa na utaratibu huo.

“Uamuzi huo utapunguza gharama za uendeshaji kwa shirika na pia kipindi cha ‘Leo katika Bunge’ Watanzania walio wengi watapata nafasi ya kufahamu yaliyojiri bungeni kwani wakati Bunge linaendelea na mijadala yake wengi huwa na kazi za kiofisi au nyingine za ujenzi wa taifa,” alisema Nape.

 

FIGISUFIGISU ZILIPOANZIA

Baada ya Nape kutoa kauli hiyo, wabunge wa upinzani walipinga na kutaka mwongozo wa mwenyekiti.

Aliyeanza kupinga alikuwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo) ambaye alisimama huku akitaja kanuni ya 69 akitaka Bunge liahirishe mjadala wa kujadili hotuba ya rais badala yake wajadili suala la kusitishwa matangazo ya moja kwa moja ya TBC.

Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bunge, Chenge alimwambia Zitto akae chini, lakini mbunge huyo aliendelea kusisitiza kusoma kanuni hiyo.

“Zitto nakusihi keti chini…hiyo kanuni haina uwezo wa kuahirisha Bunge,” alisema Chenge.

Hata hivyo Zitto alisimama tena na kusisitiza:

“Kanuni ya 69 hoja ya kuahirisha Bunge…Nashukuru kwa kutoa hoja ya kutorusha vipindi vya Bunge…” alisema Zitto na kukatishwa na Chenge aliyemwambia aisome kanuni hiyo na akakubali.

“Mbunge anayependa mjadala wowote uahirishwe anaweza na atataja mjadala huo uahirishwe na atatoa sababu kwa nini uahirishwe. Naomba kutoa sababu…” alisema Zitto, lakini Chenge akamwambia asome kifungu cha pili.

Baada ya majibizano mafupi, Zitto alikubali kukisoma kifungu hicho na baada ya kukisoma, aliruhusiwa kutoa hoja yake.

“Muda mfupi Waziri wa habari ametoa kauli inayowanyima wananchi fursa ya kufuatilia Baraza lao. TBC inaendeshwa kwa fedha za wananchi, siyo ya biashara, inafanya biashara kwa sababu Serikali haitoi fedha za kutosha.

“Rais alipohutubia wananchi ilirushwa moja kwa moja na kituo hiki, halafu wakati wa kuijadili isionyeshwe moja kwa moja, haitakuwa haki. Naomba tujadili ili tuangalie sababu za kukatisha matangazo ya moja kwa moja,” alisema Zitto huku wabunge wote wa upinzani wakisimama kumuunga mkono.

Baada ya kauli hiyo ya Zitto, Chenge alisimama na kusema kwa mujibu wa kanuni ya 49, kauli za mawaziri hazijadiliwi bungeni, lakini hata hivyo alisema hilo halimzuii mbunge kuleta hoja bungeni.

Aliwataka wabunge wa upinzani kupeleka hoja hiyo kwenye vikao vingine vya Bunge.

“Nimemsikiliza mtoa hoja kwa makini hoja yake inayoanzia kanuni ya 49, kauli za mawaziri hazijadiliwi bungeni. Lakini hilo halizuii mbunge kuleta hoja ‘substantive’ kupitia kwa katibu kwa taratibu zilizowekwa.

“Kuahirisha mjadala wa hotuba ya rais haitakuwa uendeshwaji bora wa Bunge. Naomba tuendelee,” alisema Chenge.

Hata hivyo, Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), alisimama akitaja kanuni ya 59 inayohusu haki za Bunge na kutaka kuunga mkono hoja ya Zitto.

Wakati Halima amesimama, baadhi ya wabunge wa CCM walimrushia maneno ya vijembe na kejeli na yeye akawajibu. Ndipo Chenge akaendelea kumsisitiza kwenda kuandaa hoja mahususi na wailete kwenye vikao vijavyo.

Baada ya kauli hiyo ya mwenyekiti, wabunge wengi wa upinzani walisimama na kupiga kelele kwa pamoja: “Usituburuze, usituburuze… usituburuze…”

Mambo yalionekana kumwelemea Chenge na kuwaomba wabunge wa upinzani kuketi chini.

“Wala siwaburuzi nataka niwaeleze cha kufanya, nawasihi mketi niwaambie cha kufanya… Hiyo ni hoja nzuri tu. Kutokana na uzito wa suala hili, busara ya kawaida inanituma suala hilo tulifikishe kwenye Kamati ya Uongozi wa Bunge,” alisema Chenge.

Lakini wabunge wa upinzani waliendelea kupiga kelele wakimtaka Chenge aahirishe Bunge ili kamati ya Bunge ikae.

“Mheshimiwa mwenyewe umesema hoja ni muhimu, ahirisha Bunge mkajadili,” alisikika akisema Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji (CUF).

Baada ya kuona vurugu zimeanza, Chenge aliahirisha kikao hicho.

“Kutokana na uzito wa suala hili, nasitisha shughuli za Bunge. Kamati ya uongozi itakutana kujadili suala hili kwa saa moja,” alisema.

Baada ya kauli hiyo, wabunge wa upinzani waliimba kumsifu Chenge: “Chenge… Chenge… Chenge, mtemi.”

Baada ya saa moja kupita, Chenge na baadhi ya wabunge wa upinzani walirudi bungeni kama alivyoahidi na kuahirisha vikao vya Bunge hadi saa 10 alasiri jana. Hata hivyo, wabunge wa CCM hawakurudi bungeni kwani walionekana wakiingia kwenye kikao cha chama katika Ukumbi wa Msekwa.

“Nilisitisha Bunge ili kulitafakari suala lililotokea. Suala hilo bado liko kwenye Kamati ya Uongozi. Nasitisha shughuli za Bunge mpaka saa 10,” alisema Chenge.

 

MAONI YA WABUNGE

Wakizungumzia suala hilo, baadhi ya wabunge wa kambi ya upinzani walisema Serikali ya CCM imelenga kuwanyima wananchi haki ya kupata habari.

“Huu ni uhuni tu,” alisema Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema) na kuongeza:

“Kuna mkataba kati ya Bunge na TBC kuhusu hayo malipo, na jana Nape alisema kuna tatizo la mitambo limetokea ndiyo maana hawakurusha matangazo moja kwa moja.

“Kama ni suala la bajeti angekuja na hoja ya kuongeza kwa sababu bajeti ya Serikali ilishapitishwa, atasemaje kuwa gharama imeongezeka?

“Mimi ni mbunge wa Ukonga, wananchi wamenituma hapa, wanataka wanione nikifikisha hoja zao moja kwa moja. Lakini Nape anataka yeye ndiye aratibu tunachokisema, mwisho wananchi wataona hatufanyi kazi,” alisema Waitara.

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), alisema hatua hiyo inakwenda kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano ibara ya 18 inayohusu uhuru na haki ya wananchi kupata habari.

“Hii ni hujuma kwa wabunge wa upinzani, ni kwenda kinyume na Katiba ibara ya 18,” alisema Heche.

Kwa upande wake, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), alisema utaratibu huo ni wa kidikteta.

“Huo ni ukandamizwaji wa demokrasia, huwezi kuwanyima wananchi haki ya habari kwa kisingizo cha gharama. Bunge si kama mahakama, ni chombo cha uwakilishi wa wananchi,” alisema Kubenea.

Alisema gharama zilizotajwa na Nape zinapaswa kuchunguzwa na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Hata hivyo, baadhi ya wabunge wa CCM akiwamo Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia, wamesifu utaratibu huo.

“Naipongeza Serikali kwa hatua hiyo kwa sababu baadhi ya wabunge walikuwa wakiitumia kutafuta sifa. Utakuta mbunge anawaambia wapigakura wake wamtazame atakapochangia. Hayo mambo hayapo hata kwa wenzetu, KBC Kenya hawarushi matangazo, BBC Uingereza hawarushi, sisi tuna fedha kiasi gani kurusha moja kwa moja?” alihoji Nkamia.

 

JULIUS MTATIRO

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa, Julius Mtatiro alisema hatua ya Serikali kuzuia TBC isirushe matangazo ya Bunge moja kwa moja ni dalili nyingine tosha kuwa Serikali ya sasa inao mpango kabambe wa kujiendesha kwa siri huku ikiogopa kuhojiwa.

Katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii, Mtatiro aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha Wananchi (CUF), alisema Serikali imejipanga kutumbua majipu na ilishaanza kazi hiyo, tena ikiifanya mbele ya kamera, hivyo ni ajabu leo hii kuogopa wananchi wasiwaangalie moja kwa moja kwenye luninga wawakilishi wao.

Alisema endapo Bunge litakubali kuendesha vikao vyake kwa ‘siri’ bila wananchi kuona moja kwa moja litakuwa Bunge kibogoyo kuliko yote yaliyowahi kupita, na hata Spika wa Bunge hilo, Job Ndugai atadharaulika.

“Hoja ya rafiki yangu Nape Moses Nnauye ati uamuzi huo umefikiwa ili kubana matumizi ni ya kitoto mno, hata mtoto wa chekechea hawezi kudanganyishiwa,” alisema Mtatiro.

Aliongeza kuwa inasikitisha kuona Serikali ikilalamikia gharama wakati televisheni ya Azam, ITV na wengine wanataka kurusha matangazo hayo moja kwa moja kwa gharama zao.

 

DEUS KIBAMBA

Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania (JUKATA), Deus Kibamba, alisema amesikitishwa na uamuzi huo kwani umekwishapitwa na wakati.

“Haya yanafanana na yale yanayoendelea Zanzibar kwa sababu watu wanakutana na hatujui wanaongea nini, wanaficha habari kwa sababu wanazomewa licha kuwa chanzo cha kupata habari, ukivunja haki hiyo ni hatari sana,” alisema Kibamba.

 

KIJO BISIMBA

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba alisema hoja ya kubana matumizi wakati wananchi wanalipa kodi ili wabunge waende bungeni haina mashiko.

“Sisi tunatoa kodi tumewapeleka wabunge ili watuwakilishe, na lazima tuwaone wakati wanatuwakilisha, bila kuwaona moja kwa moja haitatusaidia sisi kama jamii,” alisema Dk. Bisimba.

Alisema hoja iliyotolewa na Nape bungeni ifutwe kwa sababu wananchi wanataka kufuatilia Bunge hatua moja baada ya nyingine.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles