24 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

TACAIDS yabainisha mafanikio ya Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF)

Na Mwandishi Wetu, Mtanzania Digital

Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) imesema moja ya mafanikio yaliyopatikana ni ununuzi wa dawa (dawa za magonjwa nyemelezi), vifaa tiba na bidhaa zake (vitendanishi) sambamba na kutoa elimu ya kujikinga na VVU kwa Wanafunzi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dk. Leonard Maboko akiwasilisha mada wakati wa Semina kwa wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI iliyolenga kuwapitisha kwenye majukumu ya Tume hiyo na masuala ya UKIMWI nchini.Semina hiyo ilifanyika Bungeni jijini Dodoma.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa TACAIDS, Yasini Abbas, Aprili 14, 2023 mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala UKIMWI ikiwa ni sehemu ya kuwapitisha katika majukumu ya Tume hiyo na kuwajengea uelewa tangu kamati hiyo iteuliwe.

Amesema mbali na wanafunzi pia elimu imekuwa ikitolewa kwa  Watumishi katika vyuo vya Elimu ya Juu vya mikoa ya Dodoma na  Dar es Salaam.

Mjumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na masuala ya UKIMWI Mhe. Elibariki Kingu akichangia jambo wakati wa Semina ya masuala ya UKIMWI.

Ametaja jukumu jingine kuwa ni kufanya uraghabishi na elimu ya VVU na UKIMWI kwa vijana katika mkoa wa Tanga kwenye maeneo ambayo mradi wa bomba la mafuta ghafi linapita; kuwezesha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani.

“Moja ya mafanikio yaliyopatikana ni ununuzi wa dawa (dawa za magonjwa nyemelezi), vifaa tiba na bidhaa zake (vitendanishi) samba na kutoa elimu ya kujikinga na VVU kwa Wanafunzi.

“Pia mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI(ATF) umefanikiwa kujenga kituo cha kutolea huduma kwa watu wanaoishi na VVU –Mererani kwa lengo la  kuweka huduma karibu kwa wachimbaji madini pamoja na wakaazi wa maeneo jirani ili kuwarahisisha upatikanaji wa huduma,” amesema Abbas.

Abbas ametaja jukumu jingine kuwa ni kuratibu Mbio za Nyika (Marathon) ambazo zilifanyika wakati wa Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani mwaka 2022 mkoani Lindi kwa ajili ya kutunisha Mfuko ambapo katika mbio hizo zaidi ya Sh milioni 200 zilipatikana.

“Mafanikio hayo yametokana na jitihada za Serikali za kuanzisha Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti UKIMWI (ATF) chini ya sheria ya Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) namba 6 ya mwaka 2015 kwa lengo la kukidhi matakwa ya sera ya Taifa ya UKIMWI ya mwaka 2001 ambayo imetamka bayana kwamba Serikali itaanzisha mfuko wa UKIMWI nchini.

“Vile vile, Mfuko ulianzishwa ili kukidhi matakwa ya sheria ya UKIMWI namba 28 ya mwaka 2008 kifungu cha 4(3) kuhusu wajibu wa usimamizi wa rasilimali na mgawanyo wake katika utekelezaji wa shughuli za UKIMWI nchini,” amesema Abbas.

Aidha, amefafanua kuwa malengo makuu ya kuanzishwa kwa Mfuko wa ATF ni pamoja na kuongeza rasilimali fedha za ndani kutoka asilimia 7 (2021/2022) mpaka asilimia 30 kwa mwaka wa fedha 2025/2026 ili kupunguza utegemezi.

“Kuongeza mchango wa sekta binasfi katika udhibiti wa UKIMWI kutoka asilimia 8 mpaka asilimia 15 kwa mwaka ifikapo mwaka wa fedha 2025/2026; na kuongeza mchango wa Serikali hadi kufikia Sh bilioni 40, mwaka 2025/2026 kutoka wastani wa Sh bilioni 1.8 kwa mwaka ilivyo sasa,” amesema Abbas.

Aidha, amesema ATF inasimamiwa na bodi yenye wajumbe nane akiwemo mwenyekiti ambapo mjumbe mmoja anatoka  Wizara ya fedha, Kamisheni ya TACAIDS ,Wizara ya Afya, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI-NACP, Baraza la Watu Wanaoishi na VVU-NACOPHA, Shirika lisilokuwa la Kiserikali-NGO-, wawkilishi wawili kutoka Sekta binafsi na TAMISEMI.

“Kwa mujibu wa mwongozo wa mfuko, fedha za mfuko zitaelekezwa kwenye maeneo ya kwenye maeneo ya shughuli za tiba na uangalizi kama vile ununuzi wa dawa (dawa za magonjwa nyemelezi), vifaa tiba na bidhaa zake (vitendanishi) – 60% ambapo fedha hizi hupelekwa Wizara ya Afya kwa ajili ya ununuzi wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya matumizi ya WAVIU.

“Shughuli nyingine ni  za kinga, kama upatikanaji na  usambazaji wa kondom, uraghbishi na elimu   ya UKIMWI inayolenga kubadili tabia – 25% pamoja na Mazingira wezeshi kama utafutaji fedha, usimamizi wa programu za UKIMWI, utafiti, ufuatiliaji wa mwenendo wa UKIMWI na tahimini 15%,” amesema Abbas.       

Aidha, Abbas amesema pamoja na jitihada za kuwepo kwa mfuko lakini bado Tanzania ni moja ya nchi zinazopata ufadhili mkubwa kutoka nje katika afua za mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ambapo takribani asilimia 90 ya raslimali zinazotumika kupambana na VVU na UKIMWI zinatoka nje ya nchi kwa wafadhili na wadau wa maendeleo.

“Hili ni jambo jema kwa muda mfupi kwa muda mfupi lakini ni hatari kwa nchi katika muktadha wa muda wa kati na muda mrefu.

“Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 90 ya rasilimali zinazotumika kufadhili afua za VVU/UKIMWI nchini ni kutoka nje ya nchi (NASA 2020).

“Wafadhili wakubwa wa afua za UKIMWI nchini kwa sasa ni Mpango wa Dharura wa UKIMWI wa Rais wa Marekani (PEPFAR) na Mfuko wa Dunia wa kufadhili UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria yaani Global Fund. “Mwenendo wa michango ya wafadhili hawa inaonyesha kupungua mwaka hadi mwaka,” amesema Abbas.

Upande wao wabunge hao walishauri kuwepo na jitihada za upatikanaji wa vyanzo vya uhakika vya mfuko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles