25.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TABOA YAMPONGEZA KAMANDA MPINGA

kamanda-mpinga

Na MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM

CHAMA cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), kimelipongeza Jeshi la Polisi kwa uamuzi wake wa kupiga marufuku vyama visivyohusika kukagua magari, leseni na ratiba za safari.

Kauli ya chama hicho imekuja siku moja baada ya Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishina Mohamed Mpinga, kukipiga marufuku Chama cha Kutetea Abiria (Chakua) kufanya kazi ambazo hazikihusu kisheria.

Kamanda Mpinga alisema chama hicho kimekuwa kikifanya kazi ya ukaguzi wa leseni za madereva, ukaguzi wa magari na ratiba za safari kinyume cha sheria, jambo ambalo hutakiwa kufanywa na askari wa kikosi cha usalama barabarani (trafiki) na maofisa wa Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).

Alisema utendaji wa chama hicho umekuwa mbaya na kukiuka maadili, hasa katika Kituo cha Mabasi Ubungo na kuwataka wasijihusishe kuanzia sasa na utoaji wa sheria, bali elimu tu.

“Kuanzia sasa nasititiza utendaji wa Chakua mikoani na hasa katika vituo vya vikuu vya mabasi, watabaki katika kituo kikuu cha mabasi Ubungo tu na kule mikoani mpaka wapewe idhini ya makamanda wa polisi tu, wasijihusishe na usimamizi wa sheria.

“Tumekuwa tukipata malalamiko mengi ya utendaji usiokuwa na maadili na kuzua migogoro ya mara kwa mara kutoka kwa abiria, jana tu kwa mfano Manyara wamesababisha kiasi fulani utokee mgomo kutokana na utendaji wao,” alisema.

Alisema chama hicho kimesababisha matatizo makubwa katika mikoa ya Morogoro, Tanga na Manyara, Mbeya na  Chalinze hadi kufikia hatua ya watoa huduma ya usafiri kukusudia kugoma.

Akizungumzia suala hilo Dar es Salaam jana, Msemaji wa Taboa, Mustafa Mwalongo, alisema wamepokea kwa mikono miwili uamuzi huo ambao siku zote wameulilia.

“Tunampongeza mno Kamanda Mpinga kwa uamuzi huu, sisi tunaamini polisi ndio wamekabidhiwa kufanya kazi hizi na si watu ambao hawana elimu ya jambo fulani…tunasema tutamuunga mkono kwa nguvu zote katika kulisimamia hili.

Alisema kama hali hiyo ingeendelea, ingeweza kusababisha uhusiano kati ya Taboa na polisi kusuasua kutokana na kilio chao kutosikilizwa kwa muda mrefu.

“Tunaona tumepata mwanga mzuri wa jambo hili, imani yetu kazi zinazopaswa kufanywa na wataalamu wetu zifanywe na si kikundi cha watu wachache wasiokuwa na ujuzi wowote,” alisema Mwalongo.

Mwisho

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles