Na Elizabeth Hombo, Dar es Salaam
WAMILIKI wa Mabasi ya Abiria(Taboa) wametangaza Agosti 22 mwaka huu kuwa hakutakuwa na huduma ya usafiri wa kwenda mikoani kwa kuwa mabasi yote yatafanyiwa ukaguzi.
Ukaguzi huo utakwenda sambasamba na uhakiki wa vyeti vya taaluma na leseni za madereva wote wa mabasi hayo.
Msimamo huo ulitolewa Dar es Salaam jana na Mwenyekiti wa Taboa, Abdallah Mohamed alipozungumza na waandishi wa habari.
Alisema pia kuwa utendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) una shaka.
Mwenyekiti huyo wa Taboa alisema zaidi ya mabasi 4000 yatasimamishwa ikifika tarehe hiyo.
“Tunawatangazia wananchi wote kuwa kuanzia Agosti 22 mwaka huu hakutakuwa na usafiri wa mabasi yote kwa sababu yatakuwa kwenye ukaguzi.
“Pia madereva wote watakaguliwa vyeti vya taaluma na leseni. Chama kinawasisitiza wamiliki wote kupeleka mabasi yao kukaguliwa katika vituo vitakavyochaguliwa na serikali na kuwekwa stika,”alisema Mohamed.
Alisema msimamo huo ulitokana na maazimio ya mkutano mkuu wa wamiliki wote wa mabasi uliofanyika Agosti 16 mwaka huu.
Mwenyekiti huyo alisema wamefikia hatua hiyo baada ya kuwapo unyanyasaji ambao umekuwa ukifanywa na Sumatra.
“Tumeamua kuchukua hatua hii kwa sababu katika siku za karibuni, Sumatra wamekuwa wakifanya unyanyasaji kwa kusimamisha mabasi holela.
“Kwa mfano; mmiliki mwenye mabasi 30, lakini basi moja linaposababisha ajali baadaye mabasi yote ya kampuni yanazuiwa.
“Basi likiharibika njiani likitengenezwa na abiria kufikishwa salama lakini baadaye Sumatra wanakuja kusimamisha mabasi yote na ni kwa idhini ya waziri,” alisema.
Sababu nyingine aliyoitaja Katibu wa Taboa, Ernea Mrutu ni kuwapo wimbi la ajali ambalo limekuwa likisababishwa na magari mabovu.
“Kwa hiyo tumeamua yafanyiwe ukaguzi mabasi yote na yale mabovu yatolewe na yaliyo mazima yaachwe na kuwekewa stika na yaendelee na safari.
“Kutokana na hilo, tunasikitika sana kuwatangazia abiria ambao ni wateja wetu wajipange katika safari zao kwa sababu mwisho wa kusafirisha ni Agosti 21 mwaka huu,” alisema Mrutu.
Alisema tayari walikwisha kupeleka barua kwa Sumatra.
Akizungumzia ukaguzi wa madereva, Mrutu alisema kwa kawaida madereva huzalishwa na serikali, lakini anaposababisha ajali anayepewa adhabu ni mmiliki wa basi.
“Madereva huwa wanazalishwa na serikali na wanakaguliwa halafu wanapata leseni na sisi tunawaajiri, wanaposababisha ajali mmlilki ndiyo anapata adhabu kumbe wakati mwingine wao hawako makini,” alisema.
Mkurugenzi wa Udhibiti wa Usafiri wa Barabara wa Sumatra, Johansen Kahatano, aliupongeza uamuzi huo wa Sumatra akisema kabla ya Agosti 22 mwaka huu watakutana na Taboa kwa mazungumzo.