27.4 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

Sugu, meya mbaroni Mbeya

Joseph Mbilinyi ‘Sugu’
Joseph Mbilinyi ‘Sugu’

Na Pendo Fundisha, Mbeya

MBUNGE wa Mbeya mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ (Chadema) na Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi, wamekatwa wakidaiwa kuingilia utendaji kazi wa Jeshi la Polisi.

Viongozi hao walikamatwa jana mchana wakishutumiwa kuwazuia polisi ambao walikuwa doria wakiongozwa na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Mbeya (OCD), James Chacha.

Polisi hao  waliwakamata vibaka waliokuwa wanalalamikiwa kwa ukwapuaji  jijini Mbeya.

Viongozi hao walitiwa mbaroni walipokuwa wakiendelea na mkutano wa maendeleo katika eneo la Kabwe jijini hapa.

Polisi  walipofika eneo hilo wananchi walitaharuki kwa hofu ya kukamatwa ndipo Sugu aliposimama na kuwataka kutokimbia akisema  mkutano huo haukuwa wa siasa.

Mkutano huo ulikuwa   unaratibiwa  na Mbunge huyo,  meya, Mkurugenzi wa Jiji  na baadhi ya madiwani  na ulikuwa na lengo la kuwaeleza wananchi kuhusu mkakati wa halmashauri hiyo wa kuboresha mazingira ya wafanyabiashara wadogo  ‘Machinga’.

Wakati mkutano huo ukiendelea,   ghafla  walitokea polisi ambao baadhi yao walikuwa wakionekana kubeba mabomu ya machozi, silaha na gari la maji ya washawasha.

Walikuwa  wakikamata watu ambao kwa mujibu wa jeshi hilo,   walikuwa ni vibaka.

Kitendo hicho cha kukamata  watu  ovyo, kinadaiwa kuwa kiliwashangaza viongozi hao wa  siasa pamoja na watendaji wa halmashauri.

Hali hiyo ilisababisha Mbunge huyo  kuingilia kati na kuwataka wananchi wasikimbie, jambo lililozua taharuki kwa baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye mkutano huo.

“Tunawaomba sana ndugu zetu askari msituingilie katika mkutano huu kwa sababu  ni wa utendaji haupo kisiasa hivyo tunahitaji mtupe nafasi ili wananchi ambao ni wafanyabiashara wa eneo hili wafahamu nini halmashauri yao imewaandalia kabla ya kuwahamisha.

“… na hapa tunatekeleza agizo la Rais wa nchi  ambaye ameaagiza kutosumbuliwa kwa wamachinga mpaka watakapotafutiwa maeneo ya kuwaweka,”alisema Sugu.

Baada ya kauli hiyo, baadhi ya askari walieleza  kwamba walikuwa wametumwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Dhahiri Kidavashali, kwamba Meya na Mbunge Sugu wanahitajika katika ofisi yake.

Mbunge huyo akiwa ameongozana na   Meya wa jiji   na baadhi ya madiwani walitii agizo hilo na kwenda moja kwa moja katika ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ambako walikuwa na mahojiano maalum yaliyochukua nusu saa na kabla ya kutakiwa   kufika katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.

Akizungumzia tukio hilo, Meya Mwashilindi, alisema walikuwa katika majukumu yao ya kazi lakini walishaangaa kuona askari wakiwahitaji yeye na mbunge  Sugu kwa maelezo kwamba walikuwa wakihitajika katika ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya.

“Tulitii sheria lakini kwa masharti ya kutobughudhiwa wananchi, hivyo tulienda ofisini kwa kamanda na kumweleza lengo la mkutano huo ambako Kamanda alitutaka kwenda katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,” alisema.

Alisema wakiwa katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, walieleza kilichokuwa kikiendelea na kuonekana kwamba tatizo lilikuwa ni kushindwa kuelewana kwa pande mbili hizo na baada ya muda waliachiwa.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda  Kidavashali  alisema  jeshi hilo lilikuwa limejipanga kwa muda mrefu kudhibiti uhalifu katika eneo hilo ambalo limekuwa na matukio mengi ya uhalifu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles