24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Serikali kununua ndege nyingine mbili

Profesa Makame Mbarawa
Profesa Makame Mbarawa

Na Jonas Mushi -DAR ES SALAAM

SERIKALI imesema wiki ijayo inatarajia kutangaza tenda ya ununuzi wa ndege mbili na   ina mpango wa kuwa na ndege saba katika kipindi cha mwaka mmoja na nusu.

Pia imesema ina mpango wa kutangaza tenda ya ujenzi wa reli ya kisasa (Standard Gauge)  kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro yenye urefu wa zaidi ya kilometa 200.

Waziri wa Uchukuzi, Ujenzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, alikuwa  akizungumza na uongozi na walimu wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) baada ya kufanya ziara chuoni hapo jana.

Alisema ndege hizo zitakazokuwa na injini   ya jeti zitafanya idadi ya ndege mpya kuwa nne ambako nyingine mbili zimeshakamilika na zinatarajia kuwasili nchini Septemba 19 mwaka huu.

“Serikali hii imejipanga kuleta maendeleo makubwa katika sekta ya usafirishaji na tuna kasi kubwa katika kutekeleza hili kwa sababu  Septemba 19 mwaka huu ndege mbili aina ya Q400 zitawasili nchini na wiki ijayo siku kama ya leo (jana) tutatangaza tenda ya ndege nyingoine mbili zenye injini ya jeti,” alisema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa alisema kwa sababu hiyo NIT ni chuo muhimu na kinatakiwa kuendana na kasi ya ya maendeleo ya sekta ya usafirishaji.

“Nimegundua nchi hii haina marubani wa kutosha hivyo wakati tunahangaika kuleta ndege tunataka kuona NIT nayo inafanya jitihada za kutupatia marubani na wataalamu wengine wa usafirishaji.

“Natoa changamoto kwa chuo hiki kihakikishe kinashirikiana na mashirika ya reli kama vile TRL, TAZARA   mjue mahitaji ya huko nje badala ya kujifungia ndani peke yenu.

“Nataka mtutengenezee wataalamu watakaokubalika huko nje na si kuwa na wahitimu wenye vyeti lakini hawana utaalamu,” alisema Mbarawa.

Mkuu wa chuo hicho,   Profesa Zacharia Mganilwa, alisema  atahakikisha chuo hicho kinaendana na ukuaji wa sekta ya usafirishaji nchini kwa kuboresha miundombinu na kuongeza rasilimali watu.

“Kwa namna moja au nyingine wakati serikali inapanua miundombinu ya usafirishaji sisi tutahakikisha tunapanua chuo chetu kiweze kutoa programu nyingi na bora ili kupata wataalamu wa kuendesha sekta hizo,” alisema Profesa Mganilwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles