Na Christian Bwaya,
Tulihitimisha makala ya juma lililopita kwa kudokeza mazingira ya kimalezi yanayochangia kwa kiasi kikubwa kujenga tabia za watoto wetu. Katika makala haya tutaangalia makundi manne ya tabia za watoto zinazotokana na aina ya malezi wanayopata.
Mtoto mtulivu mwenye ukarimu
Huyu ni mtoto anayewaamini wazazi. Utulivu wake na kujiamini unatokana na kujiona yu katika mazingira salama. Si mtoto mgomvi wala msumbufu na hana tabia kulialia bila sababu. Ingawa anapofikisha umri wa miezi sita na zaidi huweza kuonesha upinzani pale mama yake anapoondoka, bado ni mwepesi kunyamaza na kutulia.
Kadhalika ni mkarimu na ana upendo wa dhahiri kwa wengine. Kadiri anavyoendelea kukua, ni mwepesi kujifunza kukabiliana na ubabe wa wenzake kwa njia za amani ikiwamo ‘nitakusemea kwa baba/mama’. Tabia hizi ni matokeo ya malezi yanayomwelewa, yanayomshirikisha, yanayokubali na kumweka karibu.
Ukiacha kundi hili, lipo kundi la watoto wenye changamoto za nafsi wasiojisikia salama kihisia waliogawanywa katika makundi madogo matatu; wanaojitenga na watu, waongeaji lakini wasiojiamini kwa siri na wale wakorofi.
Mtoto anayejitenga na watu
Huyu ni mtoto anayejiamini lakini anayejiona bora kuliko wengine. Kimsingi hajisikii salama akiwa na wengine ndio maana ana tabia ya kujilinda kwa kujitenga na wengine. Mara nyingi ni mkimya na hana muda na watu wengine ingawa anaweza kuwa na uwezo kiakili.
Akiwa mdogo, anaweza kuwa na tabia ya kutokujali pale anapoachwa na mama yake. Hata kama anaweza kulia kuonesha upinzani mama anapoondoka, lakini anaporudi, hashtuki. Kutokusisimshwa na uwepo wa mama ni namna yake ya kusema hana mahusiano ya karibu na mama yake. Tabia hii ni matokeo ya malezi yasiyojali (yanayopuuza) hisia zake ingawa yanamshirikisha kwa namna fulani.
Mtoto mwongeaji lakini asiyejiamini
Huyu ni mtoto mwenye wasiwasi na anavyojiona ingawa anawaona wengine kuwa bora kuliko yeye. Kimsingi hajiamini sana na anajiona hawezi kufanya mengi bila ‘kuzungukwa’ na watu. Kwa sababu hiyo anapenda sana kujichanganya na watu kufidia hisia za upweke ndani yake ambao si rahisi kuugundua. Wakati mwingine anaweza kuwa mpole ingawa anapokutana na watu wanaomwelewa ni mtoto mchangamfu na anaweza kuwa mwongeaji kuliko kawaida.
Huyu ni mtoto aliyeathirika na tabia ya wazazi watoro (wasiopatikana) kimwili kwa hiyo amelelewa katika mazingira ambayo wazazi wake wapo na hawapo kwa wakati huo huo. Ni mtoto anayeamini wazazi hawajali sana mahitaji yake ingawa anajua wanampenda. Hutokea wakati mwingine shauri ya kujihisi hapati ushirikiano anaoutaka hujenga hisia za kujishtukia na kujenga kisasi cha utoto.
Mtoto mkorofi/mtundu
Huyu ni mtoto asiyejielewa. Hujiona hana thamani na wengine wanaomzunguka hawana maana pia kama alivyo yeye. Ni mtoto anayejidharau na kudharau wengine. Hana hisia na haelewi hisia za wengine na ndio sababu huwa mgomvi na mtundu. Ugomvi ni namna yake ya kujitutumua kufidia uduni anaohisi ndani.
Kinachomfanya awe mgomvi ni malezi yasiyoheshimu hisia zake kama vile kuwa na wazazi wanagombana mbele yake, matusi na kukosa staha. Kadhalika, wazazi wanaoishi na hasira lakini wanaomtumia mtoto kama namna ya kujikinga na maumivu yao wanaweza kuwa sababu moja wapo.
Itaendelea
Mwandishi ni mwalimu wa Saikolojia katika Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge (MWECAU). Barua pepe: bwaya@mwecau.ac.tz, Twita: @bwaya, Simu: 0754 870 815