Na SAMWEL MWANGA- SIMIYU
TAASISI ya Benjamin Mkapa, imekabidhi majengo mawili ya upasuaji na nyumba 28 kwa Halmashauri za Mkoa wa Simiyu kwa ajili ya watumishi wa idara ya afya zote zikiwa na thamani ya Sh bilioni 1.9.
Makabidhiano hayo yalifanyika jana katika maeneo tofauti ya mkoa huu ambapo majengo mawili ya upasuaji yalikabidhiwa katika Kituo cha Afya Ngulyati katika Halmashauri ya mji wa Bariadi.
Pia sehemu ya nyumba hizo zilikabidhiwa katika Hospitali ya Mkula katika Halmashauri ya Wilaya ya Busega ambapo zilipokelewa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.
Akisoma taarifa kwa Ummy, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa, Dk. Ellen Senkoro, alisema wakati taasisi hiyo inaadhimisha miaka 10 ya kazi zao wamechangia jitihada mbalimbali za Serikali hapa nchini ikiwemo katika Mkoa wa Simiyu.
Alisema taasisi hiyo imekuwa ikitekeleza miradi mbalimbali kuanzia mwaka 2011 hadi 2016, ambayo imelenga kuimarisha mfumo wa sekta ya afya.
Alisema Taasisi hiyo mpaka sasa imejenga nyumba 480 kati ya nyumba hizo, 48 zipo katika Mkoa wa Simiyu wilaya za Busega (10), Bariadi (8), Itilima (10) Maswa (10) na Meatu (10), lakini hadi sasa tayari nyumba 28 nyingine zilikabidhiwa juzi.